Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali wa Polisi Camillus Wambura leo tarehe 18 Agosti 2022 ofisini kwa Makamu wa Rais Jijini Dar es salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali wa Polisi Camillus Wambura mara baada ya mazungumzo yao yaliofanyika ofisini kwa Makamu wa Rais leo tarehe 18 Agosti 2022 Jijini Dar es salaam.
…………………..
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali wa Polisi Camillus Wambura, Mazungumzo yaliofanyika ofisini kwa Makamu wa Rais Jijini Dar es salaam.
Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Rais amelipongeza jeshi la polisi kwa kuendelea kuimarisha amani pamoja na ulinzi wa wananchi na mali zao. Amesema kazi ya kulinda Raia na mali zao ndio msingi wa maendeleo ya nchi hii hivyo jeshi la polisi linapaswa kuendelea kuhakikisha utulivu unapatikana wakati wote.
Aidha Makamu wa Rais amelitaka jeshi hilo kutenda haki pasipo kuonea mtu yeyote na yeyote anayevunja sheria achukuliwe hatua kwa mujibu wa sheria na sio vinginevyo. Makamu wa Rais amemuagiza IJP Wambura kuangazia malalamiko yanayotolewa na wananchi kwa jeshi la polisi na kuwachukulia hatua askari wachache wanaoharibu taswira ya jeshi hilo.
IJP Wambura amefika kwa Makamu wa Rais kwa lengo la kujitambulisha mara baada ya kuteuliwa na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini.