*********************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MJUMBE wa baraza la wadhamini wa CCM Taifa, John Chiligati amewataka viongozi wapya wa CCM waliochaguliwa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wavunje makundi baada ya uchaguzi kumalizika.
Chiligati ameyasema hayo wakati akizungumza na viongozi wapya wa jumuiya za umoja wa vijana (UVCCM) wanawake (UWT) na wazazi, wa Kata za Orkesumet, Langai, Endonyongijape, Mirerani, Endiamtu na Naisinyai.
Amesema ni kawaida kuwa na makundi wakati wa mchakato wa uchaguzi ila ukishamalizika inatakiwa makundi yavunjwe.
“Wale ambao hawataki kuvunja makundi viongozi husika muwaite na kuwapa onyo ili waache mara moja kwani uchaguzi wao umekwisha,” amesema Chiligati.
Katibu wa CCM wilaya ya Simanjiro, Amos Shimba amesema chama hicho kimeshafanya uchaguzi na kupata viongozi wapya wa matawi na jumuiya za kata.
Shimba amesema wilaya hiyo ina kata 18, wana wanachama 59,568 na imeshafanya usajili wa kielektroniki kwa wanachama wake 13,000.
Amesema baadhi ya matawi ya CCM ya wilaya hiyo yana ofisi na mali mbalimbali ikiwemo maduka, mashamba na kupangisha minara ya kampuni za simu.