Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba (kulia) na Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Tanzania, Dkt. Patricia Laverley, wakisaini mikataba ya mkopo nafuu na msaada yenye thamani ya sh. bilioni 175 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kusaidia kukuza kilimo kupitia upatikanaji wa pembejeo za kilimo, jijini Dar es Salaam. Wanaoshuhudia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli (kulia) na Afisa Sheria kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bi. Angelina Chilewa (aliyesimama)
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba (kulia) na Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Tanzania, Dkt. Patricia Laverley, wakibadilishana mikataba ya mkopo nafuu na msaada yenye thamani ya sh. bilioni 175 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kusaidia kukuza kilimo kupitia pembejeo za kilimo, jijini Dar es Salaam.
Meza Kuu ikiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba (katikati-walioketi), Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Tanzania Dkt. Patricia Laverley (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli (kulia) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wawakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika AfDB, baada ya kumalizika kwa hafla ya utiaji saini wa mikataba yenye tha,ani ya shilingi bilioni 175 kwa ajili ya kuendeleza kilimo, jijini Dar es Salaam.
Meza Kuu ikiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Emmanuel Tutuba (katikati-walioketi), Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) nchini Tanzania Dkt. Patricia Laverley (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli (kulia) wakiwa katika picha ya Pamoja na Sekretarieti ya maandalizi ya mkutano huo kutoka Wizara ya Fedha na Mipango baada ya kumalizika kwa hafla ya utiaji saini saini ambapo AfDB imetoa kiasi cha sh. bilioni 175 kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kusaidia upatikanaji wa pembejeo za kilimo nchini, jijini Dar es Salaam.
(Picha: WFM – DSM)
***************************8
Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeipatia Tanzania mkopo wenye mashariki nafuu pamoja na msaada wenye thamani ya dola za Marekani milioni 75.5, sawa na shilingi bilioni 175 za kitanzania kwa ajili ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula nchini kupitia mradi wa upatikanaji wa pembejeo za kilimo.
Mikataba hiyo imesainiwa Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Emmanuel Tutuba na Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Patricia Larveley.
Akizungumza baada ya kusaini mikataba hiyo, Bw. Emmanuel Tutuba alisema kuwa kiasi cha dola milioni 73 kimetolewa kama mkopo nafuu na kiasi cha dola za Marekani milioni 2.5 ni msaada utakao tumika kuzalisha mazao ya chakula ikiwemo ngano, alizeti na mpunga.
“fedha hizi zitatumika kukabiliana na upungufu wa chakula unaotokana na athari za vita baina ya Urusi na Ukraine kwa kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo cha mazao ya kipaumbele ambayo ni Ngano, Alizeti na Mpunga kwa kuongeza matumizi ya pembejeo za kilimo kama mbolea kwa wakulima wadogo katika maeneo yaliyokusudiwa’ alisema Bw. Tutuba
Alisema kuwa kupitia mradi huo wa Kusaidia Pembejeo za Kilimo Tanzania (Tanzania Agricultural Inputs Support Project (TAISP), mambo matatu yamekusudiwa kutekelezwa ikiwemo, kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula, kutoa ruzuku ya mbolea, upatikanaji wake na matumizi ya teknolojia ya kisasa pamoja na kuboresha Sera na uwezo wa Kitaasisi.
Bw. Tutuba alibainisha kuwa Serikali inaendelea kuweka juhudi katika Sekta ya kilimo ili kuhakikisha usalama wa chakula na bei himilivu kwa wananchi wake kwa kufanya utafiti na kuboresha mbegu na kutoa ruzuku kwenye mbolea ili kuongeza uzalishaji wa chakula.
Kwa upande wake, Meneja Mkazi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Patricia Larveley, alisema kuwa mradi huo wa kuzalisha mazao ya chakula utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu katika baadhi ya maeneo yaliyochaguliwa katika mikoa ya Arusha, Dodoma, Manyara, Kilimanjaro, Mbeya, Morogoro, Njombe, Rukwa, Singida na Songwe.
Alisema kuwa matokeo yanayotarajiwa ni kuongezeka kwa zaidi ya tani milioni moja za mazao ya chakula yatakayoweza kutosheleza matumizi ya kaya milioni 1.2 ambazo ni sawa na watu milioni 4.8, wakiwemo asilimia 40 ya wanawake na vijana, pamoja na kupunguza upotevu wa mazao baada ya mavuno.
Dkt. Larveley aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa jitihada kubwa inazochukua kuendeleza mipango mizuri ya maendeleo na kuihakikishia Serikali kwamba Benki yake itaendelea kutoa ushirikiano ili kutimiza malengo yake ya kuwaendeleza wananchi wake kiuchumi na kijamii.
Akitoa shukrani zake kwa mkopo na msaada huo, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli, alisema kuwa fedha hizo zimetolewa wakati muafaka kwani Serikali imedhamiria kukuza kilimo chenye tija na kuondokana na uhaba wa chakula ikiwemo mafuta ya kula.
“Tutajenga mifumo ya kuweka uwazi wa matumizi ya fedha hizi kwa kuimarisha upatikanaji wa mbolea ambapo kila mkulima atapewa namba maalumu ya utambulisho na mfuko wa mbolea utawekwa alama maalumu ili kuzuia wezi wa mbolea na kuhakikisha unawafikia wakulima” alisema Bw. Mweli
Alisema kuwa Mradi huo utatusaidia kuzalisha mbegu hapa hapa nchini ambapo wanakusudia kuzalisha tani tani elfu tano zilizothibitishwa kitaalam na tayari taasisi kadhaa ikiwemo ASA imeanza kuzalisha mbegu hizo pamoja na kuimarisha mifumo ya umwagiliaji itakayosaidia kuzalisha mbegu mara mbili kwa msimu.
Alisema kuwa timu ya kutekeleza mradi huo imeundwa na mradi wa kuzalisha pembejeo za kilimo utaanza mara moja na kuahidi kuwa fedha hizo zilizotolewa zitatumika kama zilivyokusudiwa.