Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui akizungumza na Wabunge wa Chama cha Social Democratic Part cha Ujerumani walipofika Ofisini kwake Mnazimmoja kutaka mashirikiano katika mambo mbalimbali ya Maendeleo ya Afya .
Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Nassor Ahmed Mazrui (KULIA) akimkabidhi zawadi maalum Mbunge wa Chama cha Social Democratic Part cha Ujerumani Tina Rudolph wakati alipofika Ofisini kwake Mnazimmoja kuendeleza mashirikiano Kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Ujerumani .PICHA NA FAUZIA MUSSA- MAELEZO ZANZIBAR
……………………………….
Na Rahma Khamis Maelezo Zanzibar
Waziri wa Afya Zanzibar Mhe, Nassor Ahmed Mazurui Amesema kuwa Serikali ya Ujerumani imekusudia kuanzisha mfuko wa bima ya Afya (Health Insuarence) ambao utasaidia wananchi kuwapunguzia gharama za matibabu na kuweza kupata huduma bora Nchini .
Ameyasema hayo huko Ofisini kwake Mnazimmoja wakati alipotembelewa na wabunge wa chama cha Social Democratic Part cha Ujerumani kujadili namna ya kupunguza na kumaliza maradhi mbalimbali ikiwemo Kifua Kikuu,HIV,Homa ya Ini na Malaria.
Amesema kuwa ni muhimu sana kutumia bima kwani kutasaidia kuinua hali za wanyonge ambao hawawezi kumudu gharama kubwa za matibabu hivyo kutawezesha kupunguza ugumu wa gharama za matibabu kwa wananchi wa Zanzibar.
Aidha Mhe.Mazrui amefahamisha kuwa ushirikiano uliopo kati ya Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Ujerumani unazidi kuimarisha sekta ya Afya Nchini kwani umesaidia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza maradhi mabalimbali.
“ ujio wa Wabunge hawa utaimarisha mashirikano kati yetu na Wajerumani na utasaidia zaidi kuimarisha Sekta ya Afya katika kukabiliana na Maradhi mbalimbali, endapo tutauzinduwa mfuko huu utatuinua kimatibabu kwani Wananchi wengi hatumudu gharama kubwa za matibabu”.alisema Waziri huyo.
Hata hivyo Waziri Mazrui amewahakikishia wabunge hao kuwa msaada wao wanaoutoa unatumika vizuri katika kuimarisha matibabu kwa kununua vifaa tiba ambavyo vinasaidia wagonjwa na wananchi kwa ujumla.
Nao wabunge hao wameahidi kuendeleza ushirikiano wao kwa lengo la kustawisha afya za wananchi wote wa Zanzibar.
Tokea 2002 Ujerumani imeanzisha ushirikiano na Zanzibar ambapo ilianzisha mfuko wa( Global Fund) unaosaidia kupambana na maradhi mbalimbali Nchini.