![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2022/08/IMG-20220816-WA0134-1024x461.jpg)
Afisa mhamasishaji kitengo cha damu salama ofisi za kanda Burton Mbega akizungumza na Fullshangwe Blog mara baada ya kukamilisha zoezi la uchangiaji damu kwa wahitimu wa kidato cha sita waliohitimu mwaka huu.
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2022/08/IMG-20220816-WA0131.jpg)
Fortunatus Msimo ambae ni muhitimu wa kidato cha sita katika shule ya Sekondari Mkolani iliyopo Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza akichangia damu katika ofisi ya kanda ya damu salama
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2022/08/IMG-20220816-WA0132-1024x461.jpg)
Wahitimu wa kidato cha sita waliohitimu mwaka huu katika shule mbalimbali Mkoani hapa wakijaza dodoso kwaajili ya kuweka taarifa zao kabla ya kuchangia damu
………………………………
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Wahimu wa kidato cha sita waliohitimu mwaka huu kutoka katika shule mbalimbali Mkoani hapa wamechangia damu katika ofisi ya kanda ya damu salama kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa na wenye uhitaji wa damu.
Wahitimu hao wamechangia damu leo Jumanne Agositi 16,2022.
Akizungumza na Fullshangwe Blog Afisa mhamasishaji kitengo cha damu salama kutoka katika ofisi za kanda Mkoani Mwanza Burton Mbega,amesema wahitimu hao wamefanya kitu kizuri na cha kizalendo kwani mchango wao wa damu walioutoa utakwenda kuokoa maisha ya watu wengi.
Mbega amesema uhitaji wa damu katika ofisi ya kanda ya damu salama ni mkubwa sana kwani kwa mwezi wanatakiwa kukusanya chupa 1,333 lakini hadi sasa kwa mwezi huu wa Agositi wamekusanya chupa 400.
“Tunafanya jitihada kubwa sana ya kuhimiza watu kuchangia damu sanjari na kutoa elimu ili kuweza kufikia lengo la kukusanya chupa 1,333 kwa mwezi huu,hivyo tunawaomba sana Wananchi wajitolee kuchangia damu ili kwa pamoja tusaidiane kuokoa maisha ya wenye uhitaji”,amesema Mbega
Amesema mtu anapochangia damu chupa moja inasaidia kuokoa watu watatu,na uchangiaji damu kutoka kwa wadau mbalimbali unasaidia kuokoa maisha ya Watoto,kina mama,wajawazito,watu waliopata ajali pamoja na watu wenye uhitaji.
Kwa upande wake Fortunatus Msimo,ambae ni muhitimu wa kidato cha sita katika shule ya Sekondari Mkolani iliyopo Wilaya ya Nyamagana Mkoani Mwanza amesema amechangia damu ili kusaidia Watoto wenye umri chini ya miaka mitano pamoja na makundi mengine ya wagonjwa.
“Mimi ni mara yangu ya tatu kuchangia damu naninaamini kabisa unapochangia damu unakuwa umeokoa maisha ya wagonjwa wanaohitaji kuongezewa damu,hivyo nitoe wito kwa vijana wenzangu kuwa na moyo wa kujitoa kwaajili ya wenye uhitaji”,amesema Msimo
Naye Neema Juliani amesema kuna umuhimu mkubwa sana wa kujitoa katika kuchangia damu kwani hakuna mbadala mwingine wa kupata damu zaidi ya watu kuchangia hivyo ameiomba jamii kuwa na muamuko mkubwa katika suala hilo.