Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amewataka makarani na wasimamizi
wa sensa mkoani hapa kulifanya zoezi la kitaifa la sensa ya watu na makazi kwa
uwedi na umakini wa hali ya juu.
Serukamba ameyasema hayo leo Agosti
15, 2022 wakati akizungumza na makarani na wasimamizi hao ambao
wanaendelea na mafunzo katika Shule ya Sekondari ya Mwenge mjini Singida.
Alisema jukumu walilonalo nalo ni kubwa kubwa mno hivyo wanatakiwa
kuhifanya kazi hiyo kwa weledi na umakini mkubwa na sivinginevyo.
“Jukumu mlilopewa ni kubwa sana mnahitajika kulifanya kwa umakini ili taifa
lipate takwimu sahihi za watu kwa ajili ya kupanga mipango ya maendeleo kuanzia
ngazi ya chini” alisema Serukamba.
Serukamba aliwataka makarani hao kuzingatia yale yote wanayofundishwa
badala ya kuwazia kupata posho jambo ambalo sio zuri.
“Zoezi hili la sensa la kitaifa ni kubwa na linahitaji umakini wa hali
ya juu na watakalofanya lifanikiwe ni nyie hivyo msilifanye kama ni la kuja
kutafuta posho,inawezekana wengine wapo hapa na vishikwambi anayofundishwa
haelewi anachokifikiria ni kupata hela tu hii utakuwa hujaisaidia nchi
yako,” alisema.
Serukamba alisema kupitia sensa hii nchi itaweza kujua idadi ya maskini,
watu wanahitaji shule,afya na maji kiasi
gani hivyo vijana watambue wameaminiwa na nchi waifanye kazi ya sensa kwa
umakini sana.
Alisema mtihani kwa wasimamizi na makarani wa sensa ni kuifanya kazi kwa
weledi na kuleta takwimu sahihi ambapo wakiifanya vizuri kazi hii serikali
itakapokuwa na kazi nyingine wao ndo watapewa kipaumbele kupewa.
“Mkoa unawategemea sana kupata takwimu sahihi na kuufanya uwe miongoni
mwa mikoa itakayofanya vizuri katika zoezi la hili la sensa ambalo hufanyika
kila baada ya miaka 10,” alisema.
Serukamba alisema makarani na wasimamizi watapewa madodoso hivyo ni muhimu
wajifunze mbinu za kuwauliza wananchi ili kuwafanya wawaelewe watakapokuwa
wakiwadadisi.
“Kuja mtu unaweza kumuuliza una ng’ombe wangapi akashindwa kueleza
pengine akidhani unataka kuja kunyang’anya ng’ombe wao …hapana ni muhimu
kujifunza mbinu za kumfanya mtu akuelewe sababu majibu yenyewe yanatokana na
maswali rahisi atakayoukuzwa,” alisema.
Aliongeza kwa mfano Tanzania inaelezwa ni nchi ya pili katika Afrika kwa
kuwa na mifugo mingi baada ya Ethiopia lakini ukiuliza tuna ng’ombe au mbuzi
wangapi hakuna anayejua.
Alisema sensa inakwenda kuleta majawabu yote hayo kinachohitajika ni
umakini kwa makarani na wasimamizi wa Sensa ya Watu na Makazi walioaminiwa na
serikali kuifanya kazi hiyo.
Mratibu wa Sensa ya Watu na Makazi Mkoa wa Singida,Naing’oya Kipuyo alisema makarani 445 wamehitimu mafunzo yao ya dodoso
la sensa ambalo watahoji majengo na makundi maalum.
Alisema kundi la pili ni la wasimamizi wa maudhui ambao watahoji dodoso la
jamii ambao wapo 212 ambao wataendelea na mafunzo kwa siku tatu.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba alizungumza na makarani hao muda
mfupi baada ya kuukabidhi Mwenge wa Uhuru 2022 kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma baada
ya kumaliza mbio zake mbio zake mkoani hapa na kuridhishwa na miradi yote ya maendeleo iliyokaguliwa yenye thamani ya Sh.8.2 Bilioni.