MAFUTA YA KUPIKIA
Waziri Kijaji amesema Serikali inatekeleza Mkakati wa kuongeza uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kula ikiwa ni pamoja na kuhamasisha wakulima kutumia mbegu bora za alizeti na chikichi (mawese) ili kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kupikia yatokanayo na mazao hayo.
“Ongezeko la bei ya mafuta duniani lina athari hasi kwetu Watanzania, kwani mahitaji ya mafuta ndani ya Taifa letu kwa mwaka ni tani 650,000 (MT) huku uwezo wetu wa kuzalisha mafuta ni tani 270,000 (MT), ambayo ni sawa na asilimia 41.5 tu ya mahitaji yetu kwa mwaka,”amesema.
SABUNI
Amesema kuwa bei za sabuni za kufulia za mche zimeongezeka katika kipindi cha mwezi Agosti kutokana na kuongezeka kwa bei ya malighafi za kutengeneze sabuni zinazoagizwa kutoka nchi za Indonesia na Malaysia.
”Bei zimepanda kutoka wastani wa Dola za Marekani 500 hadi 600 kwa tani hadi Dola za Marekani 1,800 kwa tani, hasa baada ya nchi ya Indonesia kuweka zuio la kusafirisha nje malighafi hizo. Kutokana na ongezeko hilo la bei ya malighafi bei kwa mche ni kati ya Shilingi 3,000 na 4,500.”amesema
Vilevile,amesema sabuni ya kufulia ya unga inauzwa kwa shilingi 1000 hadi 4500/- kwa kilo moja (Doffi, Niceone, Killsoft) wakati Omo ikipatikana kwa Shilingi 8000 hadi 8200/- kwa kilo moja.
NGANO
Dk.Kijaji amesema Serikali inatekeleza Mkakati wa kuongeza uzalishaji wa zao la ngano nchini ili kukabiliana na upungufu wa tani 800,000 tunazoagiza kila mwaka huku kiasi kikubwa kikitoka katika nchi za Urusi na Ukraine.
”Mahitaji ya ngano nchini ni tani 1,000,000 kwa mwaka huku uzalishaji wa ndani ukiwa chini ya tani 200,000 kwa mwaka. Kwa mwezi Julai, bei ya kilo moja ya ngano hapa nchini ni wastani wa Shilingi 2,000 na kwa mikoa ya pembezoni hadi Shilingi 4,000 kwa kilo moja. Aidha, bei hii haikubadilika kwa mwezi Agosti.”
VIFAA VYA UJENZI
SARUJI
Amesema kwa sasa nchi ina jumla ya Viwanda 17 vya Saruji vyenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya saruji hapa nchini.
Aidha amesema kuwa Wastani wa bei ya saruji kwa mwezi Julai ilikuwa kati ya Shilingi 14,500 na 16,500 kwa mfuko wa Kilo 50 wa Saruji ya 32.5R na Shilingi.17,200 hadi 23,000 kwa saruji ya 42.5N. Wastani wa bei ya saruji kwa mwezi Agosti ni Shilingi 14,500 kwa Saruji ya 32.5R na Shilingi. 17,000 kwa saruji ya 42.5N.
NONDO
Amesema kuwa nchi ina jumla ya Viwanda kumi na sita (16) vyenye uwezo wa kuzalisha tani 1,082,788 za nondo kwa ukubwa wa 16mm, 12mm, 10mm na 8mm. Hata hivyo, kwa sasa uzalishaji wa nondo ni tani 750,000.
”Wastani wa bei ya nondo za 16mm ni kati ya Shilingi 45,000 na 52,000 kwa mwezi Julai; na Shilingi 41,000 hadi 55,000 kwa mwezi Agosti kutokana na umbali kutoka viwandani na ongezeko la gharama ya usafirishaji na bei ya dizeli. Wastani wa bei ya nondo za 12mm ni kati ya Shilingi 24,500 na 30,000 kwa mwezi Julai na Shilingi 24,000 hadi 30,000 kwa mwezi Agosti, 2022.”
Hata hivyo amesema wastani wa bei ya nondo za 10mm ilikuwa kati ya Shilingi 19,000 na 23,000 kwa mwezi Julai na Shilingi 18,000 hadi 23,000 kwa mwezi Agosti; 2022. Wastani wa bei ya nondo za 8mm ilikuwa Shilingi 14,500 hadi 19,500 kwa mwezi Julai na Shilingi 10,000 hadi 18,000 kwa mwezi Agosti, 2022.
BATI
Waziri amesema Mwezi Julai, 2022 bati za gauge 28 iliuzwa kwa wastani wa Shilingi 30,000 hadi 45,000 na mwezi Agosti inauzwa kati ya Shilingi 30,000 hadi 45,000.
”Wastani wa bei ya bati za gauge 30 kwa mwezi Julai ziliuzwa kati ya Shilingi 22,000 hadi 28,500 na mwezi Agosti zinauzwa kati ya Shilingi 22,000 hadi 28,000. Wastani wa bei kwa bati za gauge 32 kwa mwezi Julai ilikuwa kati ya Shilingi 19,000 na 26,000 na mwezi Agosti ni kati ya Shilingi 18,500 na 26,000.”
SUKARI
Amesema kuwa mahitaji ya Sukari nchini kwa mwaka 2021/22 ni wastani wa tani 655,000 ambapo kati ya hizo, tani 490, 000 ni kwa matumizi ya kawaida na tani 165,000 ni kwa matumizi ya viwandani.
”Uzalishaji wa sukari kwa viwanda vya ndani unakadiriwa kuwa kiasi cha tani 394,606 ambayo ni sawa na asilimia 80.5 ya mahitaji ya sukari nchini kwa matumizi ya kawaida. Aidha, nchi yetu ina jumla ya viwanda 5 vya kuzalisha sukari. Kila mwaka tunalazimika kuagiza sukari kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuziba pengo la uzalishaji (Sugar gap)”
Waziri Kijaji amesema kuwa Katika kipindi cha mwezi Julai na Agosti 2022, bei ya rejareja kwenye maeneo mengi nchini ni kati ya Shilingi 2,400 na 3,000 kwa kilo. Maeneo machache hasa ya pembezoni ni shilingi 3,000 kwa kilo kutokana na ongezeko la gharama za usafirishaji.
BIDHAA ZA VYAKULA
MAHARAGE
Amesema kuwa Maharage katika masoko yanapatikana kwa wastani wa bei ya Shilingi 1,800 hadi 2,600 kwa kilo. Bei hiyo ni ongezeko la kutoka Shilingi 1,650 hadi 2,600 kwa kilo mwezi Julai, 2022.
MCHELE
Amesema kuwa wastani wa bei ya mchele kwa kilo ni kati ya Shilingi 1,700 na 3,000 katika maeneo mbalimbali nchini kwa mwezi Agosti. Bei hii ni ongezeko la asilimia saba kutoka wastani wa Shilingi 1,600 hadi 2,800 kwa kilo mwezi Julai, 2022.
MAHINDI NA UNGA WA MAHINDI
Dk.Kijaji amesema kuwa bei ya zao la mahindi kwa kilo moja haikuonesha mabadiliko yoyote kati ya mwezi Julai na Agosti, 2022, ambapo zao hilo linauzwa kwa Shilingi 700 hadi 1,500 kwa kilo. Unga wa Mahindi unapatikana kwa Shilingi 1,400 hadi 1,700 kwa kilo mwezi Agosti, kutoka bei ya mwezi Julai ya Shilingi 1,100 hadi 1,700.
ULEZI
Waziri amesema kuwa wastani wa bei ya ulezi ni Shilingi 1,200 hadi 3,000 kwa kilo kwa mwezi Agosti na hakuna mabadiliko ya bei kutoka mwezi Julai, 2022.
UWELE
Waziri Kijaji amesema kuwa wastani wa bei ya uwele ni Shilingi 1,200 hadi 3,000 kwa kilo mwezi Agosti 2022; na hakuna mabadiliko ya bei za mwezi Julai, 2022..
VIAZI MVIRINGO
Waziri Kijaji amesema kuwa wastani wa bei ya viazi mviringo ilikuwa Shilingi 800 hadi 1,500 kwa kilo mwezi Julai, 2022; na Shilingi 900 hadi 1,400 kwa mwezi Agosti, 2022..
FURSA ZA MASOKO YA BIDHAA ZINAZOZALISHWA NCHINI
Waziri ameeleza kuwa Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kutafuta masoko ndani na nje ya nchi kwa ajili ya mazao na bidhaa zinazozalishwa nchini.
”Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara inaunga mkono jitihada za Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan za kuifungua nchi, kuvutia uwekezaji na utalii kwa kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa nchini. ”amesema Dk.Kijaji