Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabishara, Viwanda,na Kilimo TCCIA Mkoa wa Mwanza Gabriel Chacha (Katika) akitoa taarifa ya kuanza kwa maonesho ya biashara ya Afrika Mashariki kwa waandishi wa habari
Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabishara, Viwanda, na Kilimo (TCCIA)Mkoa wa Mwanza Gabriel Chacha akizungumza na waandishi wa habari juu ya maonesho ya biashara ya Afrika Mashariki yanayotarajiwa kuanza Agositi 26 mwaka huu
**************************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Maonesho ya 17 ya biashara Afrika Mashariki yanatarajiwa kuanza kufanyika Agositi 26,2022 hadi Septemba 4 mwaka huu katika uwanja wa Nyamagana Jijini Mwanza.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Jumatatu Agositi 15,2022 Mwenyekiti wa Chemba ya Wafanyabishara,Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Mwanza Gabriel Chacha,amesema malengo ya maonyesho hayo ni kufungua fursa kwa wafanyabiashara wa kada zote ili kuweza kukuza uchumi wa Taifa.
“Maonesho haya yanatoa fursa kwa makampuni mbalimbali Afrika Mashariki kwa kujitangaza, wafanyabiashara kuongeza mtandao wa biashara,kuongeza ubora wa bidhaa na kuboresha teknolojia,kutafuta wabia wapya wa kibiashara pamoja na kufanya utafiti wa masoko”,amesema Chacha
Ameeleza kuwa mwaka jana walialika washiriki 300 waliofika ni 180 kutokana na changamoto ya ugonjwa wa corona ambapo amesema mwaka huu wamealika washiriki 350 kati ya hawo 50 ni kutoka nje ya nchi.
Chacha amesema bidhaa zitakazooneshwa kwenye maonesho hayo ni bidhaa za mashine na teknolojia,bidhaa za ujenzi thamani za nyumba na ofisini,kilimo na mifugo,usindikaji na vinywaji,bidhaa za nguo na ngozi,bidhaa za sanaa na kazi za mikono,bidhaa za mawasiliano ya habari pamoja na bidhaa za utalii na maliasili ili kutangaza utalii wa Tanzania na vivutio vilivyopo Mkoani Mwanza.
Aidha,Chacha ametumia fursa hiyo kuishukuru Serikali kwa kuufanya Mkoa wa Mwanza kuwa kitovu cha biashara kwa kutengeneza mazingira mazuri ya miundombinu hali inayopekekea kuchochea kasi ya maendeleo.
Mwisho amewakaribisha Wananchi wote kuja Mwanza kwaajili ya kutembelea maonesho hayo ili waweze kujifunza mambo mbalimbali yatakayowasaidia kujikwamua kiuchumi.