Naibu Waziri Jumanne Sagini akizungumza na abiria waliopata ajali ya basi la Shaloom Express iliyotokea jirani na Daraja la Mto Wami,mkoani Pwani 13/08/2022.
Naibu Waziri Jumanne Sagini akikagua na basi la Kampuni ya Shaloom Express lililopata ajali jirani na Daraja la Mto Wami,mkoani Pwani
……………………………………
Na Mwandishi wetu,
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Jumanne Sagini amesikitishwa na ajali ya basi la Kampuni ya Shaloom Express linalotoka jijini Arusha kuelekea Dar es Salaam iliyotokea jana Agosti 13 jirani na Daraja la Mto sambasamba na ajali nyingine zinazojitokeza nchini kwa ujumla na kuwataka abiria wanaotumia vyombo vya moto vinavyosafiri masafa marefu kutoa taarifa mapema kwa askari Polisi wa usalama barabarani endapo watakapoona basi au chombo chochote cha usafiri kinahitilafu ili kuepuka ajali.
Akizungumza na abiria walionusurika katika ajali hiyo, Naibu Waziri Sagini amesema kuwa ni wajibu wa kila mwananchi kujilinda na ajali zinazotokea barabarani na kusema kuwa wakiona hitilafu yoyote kwenye chombo wanachosafiria na dereva mwenyewe basi ni bora kutoa taarifa mapema kwa askari polisi wa usalama barabarani ili hatua zingine zichukuliwe.
“Tunashukuru Mungu kwamba abiria wote wametoka salama na ni wape pole sana abiria waliojeruhiwa. Naomba mtambue kuwa Serikali ipo pamoja nanyi na niwaombe abiria watusaidie kuwa walinzi wa usalama wao wenyewe.Toeni taarifa endapo mnaona basi linahitilafu”
Aliyasema hayo jana, Agosti 13, 2022 baada ya kukagua basi lililopata ajali jirani na Daraja la Mto Wami la Kampuni ya Shaloom Express linalotoka jijini Arusha kuelekea Dar es Salaam.
Aidha Naibu Waziri Sagini amemuagiza Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani kuhakikisha mizigo yote ya abiria ya waliojeruhiwa ambayo imebaki inahifadhiwa ili waweze kupata mizigo yao.
Mmoja wa manusura katika ajali hiyo aliyefahamika kwa jina la Shaban Abdala aliishukuru Serikali kwa kujitokeza mapema na kusema gari hilo lilikuwa bovu na kwamba baadhi ya abiria waliokuwa ndani ya basi hilo walikuwa wakilalamika uchakavu wa gari hilo.
“Naishukuru Serikali kwa kujali na kujitokeza mapema na basi hilo lilianza kuwa na tabu ya usalama kuanzia mapema na kwamba lilifikia hatua kwenye mlima ilishindwa kupanda.”