Adeladius Makwega –Chamwino –DODOMA
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Talama, wilayani Chamwino mkoani Dodoma, ndugu Andason Makolokolo amewataka wananchi wa eneo hilo watoe ushirikiano kwa makarani wa sensa, kwa maana kilichoonekana wakati wa sensa ya majaribio Agosti 12, 2022 kwa baadhi wa wananchi wa mtaa huo hawakutoa ushirikiano.
“Jana kulikuwa na sensa ya majaribio, wale wasimamizi wamenipa taarifa walipofika nyumbani kwenu mlijifungia milango na wengine kuondoka kabisa. Jamani ndugu zangu tusionekana tuko dunia ya wapi, sensa hii siyo ya mwaka huu tu, hata ukisoma kwenye biblia ipo, isije ikafika Agosti 23, 2022 wewe ukaona makarani ukafunga mlango tena, tutakuchukulia hatua. Nawaombeni hiyo dhana muondokane nayo.”
Mwenyekiti huyo wa mtaa aliyasema haya mapema Agosti 13, 2022 katika zoezi maalumu la kuyafanyia usafi maeneo ya makaburi yaliyopo katika eneo la Malecela kando na Ikulu ya Chamwino, huku watu kadhaa wakijitokeza kufanya usafi huo
Akizungumzia zoezi hilo la usafri wa makaburi mwenyekti Makolokolo alisema kuwa ni muhimu kila mmoja wetu kushiriki shughuli za maendeleo pahala alipo, awe mwenye nyumba au mpangaji kwa kuwa maendeleo hayawatengi watu bali yanawaunganisha .
“Makaburi haya tunazika sote, wapangaji na wenye nyumba, wenyeji na wageni, natambua baadhi ya wageni wanaweza kudhani akipata msiba atazikwa kwao, hilo ni sawa, lakini kuna wakati hali ya maiti inakulazimisha kuzika eneo ilipo maiti kwa wakati huo. Hata sisi tumezika sana ndugu zetu katika maeneo mbalimbali ya nchi hii. Kwa hiyo nawaombeni kila mmoja wetu ashiriki shughuli kama hizi na zoezi hili ni endelevu.”
Mwandishi wa habarii hii alishuhudia wakazi wa eneo hilo walipokuwa wanalima eneo hilo hawakujali dini au madhehebu bali makaburi yote, ikisisitizwa majani yanayochomwa yachomwe kwa umakini kuepusha malalamiko ya makaburi kuungua kwa moto.