NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu utekelezaji wa vipaumbele vya sekta ya maji kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
……………………………..
Naibu Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema Serikali imepanga kutekeleza jumla ya miradi 1029 ya maji vijijini ambapo miradi 648 ni miradi inayoendelea kutekelezwa na miradi 381 ni mipya. Aidha, miradi 175 imepangwa kutekelezwa maeneo ya mijini.
Mheshimiwa Mahundi amesema hayo wakati akieleza vipaumbele vya sekta ya maji jijini Dodoma kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Amesema wizara ina matumaini makubwa kufikia malengo kutokana na uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameonesha nia ya dhati ya kuhakikisha mama wa Kitanzania anatuliwa ndoo ya maji kichwani.
“Ifikapo 2025 Wizara imepanga kutekeleza jumla ya miradi 1029 ya Maji ambapo miradi 648 ni miradi inayoendelea kutekelezwa na miradi 381 ni mipya”,amesema Mhandisi Mahundi
Kuhusu ubora wa maji yanayopelekwa kwa wananchi amesema kuwa Wizara kupitia maabara zake 17 za ubora wa maji nchini itaendelea kuhakiki na kufuatilia ubora wa maji katika vyanzo vya maji na mitandao ya kusambaza maji mijini na vijijini kwa lengo la kuhakikisha watumiaji wa maji wanapata huduma ya maji yanayokidhi ubora.
“Matumaini yetu ni kuhakikisha maagizo tuliyopewa kupitia Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi inafikiwa.”
Amesema kuwa Wizara ya Maji imeidhinishwa jumla ya shilingi 709,361,607,000 kwa ajili ya matumizi na kati ya fedha hizo, matumizi ya kawaida ni shilingi 51,462,269,000 ambapo shilingi 16,700,534,000 ni kwaajili ya kugharamia matumizi mengineyo.
“Sote tunajua kwamba bila Maji hakuna uhai hivyo utekelezaji wa shughuli zozote zinazolenga kuboresha uwepo wa Maji, upatikanaji wake kwa matumizi mbalimbali pamoja na ubora stahiki ni kipaumbele cha kudumu kwenye mikakati ya Wizara na Serikali kwa ujumla”, amesema
“Vipaumbele vya Wizara kwa Mwaka 2022 na 2023 ni pamoja na kukamilisha ujenzi, ukarabati na upanuzi wa Miradi uayoendelea kutekelezwa kuanzia ujenzi wa mabwawa ya kimkakati ya Kidunda na Farkwa, na kuanzia ujenzi wa Miradi ya maji mipya ikiwemo Miradi ya Maji katika Miji 28”.Amesema Mahundi
Aidha amesema Rasilimali za mani zilizopo Nchini zinakadiriwa kuwa mita za ujazo bilioni 126 kwa Mwaka zikiwemo bilioni 105 juu ya ardhi na bilioni 21 chini ya ardhi.
“Serikali katika Mwaka 2022 na 2023 itaendelea kuwekeza katika utunzaji wa vyanzo vya maji pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na kuboresha ufanisi katika matumizi ya Maji kwa lengo la kuepusha nchi kuwa na uhaba wa Maji”, amesema
” Lakini pia Usimamizi na ubora wa Maji ni moja walo ya masuala muhimu katika maendeleo ya Taifa letu katika kukinda afya ya Jamii,mazingira na vyanzo vya Maji”. Amesema Mahundi
Ameongezea kwa kusema kuwa upatikanaji wa huduma ya Majisafi na salama kwa Wananchi waishio Vijijini inafikia zaidi ya asilimia 85.