Adeladius Makwega –CHAMWINO
Agosti 12, 2022 majira ya mchana nilikuwa nyumbani kwangu naandaa chakula changu cha mchana , huku nikizungumza na jamaa zangu katika simu ya mkono, gafla nikasikia sauti ya ya mtu akibisha hodi , niliikata simu na kujibu, karibu. Nilipotoka nilikutana na binti mdogo aliyevali suruali ya rangi nyeusi na blauzi yenye maua maua.
Alinisalimu na mimi kuitikia salamu hiyo, akasema meneno haya,
“Mimi ninaitwa Jean Weston, tunafanya majaribio ya sensa kwa hiyo tunapita hapa nyumbani kwako, ninaomba ushirikiano .”
Nilimjibu hakuna neno, na kumchukua hadi katika benchi langu maalum, nilipomtazama binti huyu alilingana fika na binti zangu, nilimkaribisha binti huyu katika benchi langu ninaloliita benchi la ujamaa, maana bechi hilo hakaribishwi kila mtu bali, wale wajamaa wezangu tu. Kwa kuwa binti huyu alikuwa anafanya jambo la kijamaa alikaribia. Tukawa tunatazamana
Alianza kuniuliza maswali kadhaa, huku nikitoa majibu na yale majibu yangu akiyaweka katika kifaa kilichofanana na simu ya janja mkononi mwake.
Akaniuliza sasa mzee wewe hapa unapikia nishati gani? Nikamjibu napikia gesi lakini gesi yangu ikisha napikia mkaa, kuni na mara moja moja umeme. Lakini huu umeme na gesi bei kubwa na ndiyo maana hapa nimepanda miti, nikikwama kuni zipo, akawa anajaza majibu katika kifaa chake huku anacheka.
Wakati najibu swali hilo nikakumbuka kuwa jikoni kwangu nimebandika wali, nikamuomba samahani nikaenda kuipua wali wangu mekoni.
Niliporudi nakaulizwa swali lingine, Nini chanzo kikuu cha maji katika kaya hii? Nikamjibu hapa bomba. Swali hilo lilinishitua mno. Kwa kuwa liliishia hapo. Akaendelea na maswali mengine, alipoanliza nikamwambia mwanangu hapa bomba lipo lakini wiki nzima maji hayatoki nimechota maji kisimani . Lakini haya maji ya bomba yana chumvi hayafai kwa kunywa, huwa nanua maji ya chupa kila siku. Majirani zangu wengine wanaoshindwa kununua maji ya chupa wanachota maji ya kisima na kuyachemsha na kunywa .
Hapa tukawa tunaongea kirafiki na huyu binti, nikamuuliza hapo majibu yetu yanayotajiwa yawe nini?
“Maji ya bomba/mfereji eneo la nyumba, Maji ya bomba /mfereji jamii, Kisima cha maji au cha pampu jamii, Kisima kilichochimbwa katika kaya hii, chemichemi mfereji uliojengwa katika makazi, maji ya mvua, maji ya chupa, pikipiki/ guta, gari.”
Kwa hali ilivyo haya majibu yote yanakubalika mathalani kwangu mimi , nina bomba ikianza mvua kunyesha sinunui maji ya chupa nakinga ya mvua nakunya. Tukaagana na mgeni wnagu na huyu binti kwenda zake.
Nikabaki mwenyewe nikajiuliza je swali hili serikali itapata majibu yatakayokuwa na tija baadaye?
Aliyetengeneza swali hili alitakiwa kwenda mbali zaidi, Kwa mfano je maji hayo yanayotoka katika bomba ni ya chumvi? Ya magadi? Maji makali au maji matamu ? Je maji hayo unayatumia kwa kunywa?
Ndugu hawa wa sensa wangeweka swali hilo namna hivyo wangeweza kupata takwimu kuwa katika baadhi ya maeneo yapo maji ya bomba lakini hayatumiki kwa kunywa, kwa hiyo kunahitajika kutafutwa vyanzo vingine vya maji ambayo yatafaa kwa kunywa. (Hayana magadi, hayana chumvi na si maji makali)
Hawa ndugu zangu akiwa Uwesu watapanga bajeti ambayo takwimu zitaonesha shida hiyo ilipo.
Mwanakwetu huyu mtunzi wa swali anauliza kwa dhana kwa kuwa yeye kama haifahamu jamii ya Kitanzania. Nashauri sensa ni Agosti 23, 2022 swali la maji liboreshwe .