Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja,akizungumz na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Agosti 13,2022 jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2022-2023.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja,akisisitiza jambo kwa na waandishi wa habari leo Agosti 13,2022 jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2022-2023.
……………………………………….
Na Alex Sonna-DODOMA
SERIKALI kupitia Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kutenga sh. trilioni 1.029 kutekeleza miradi ya maji 13 ya kimkakati katika mwaka wa fedha 2022/2023.
Hayo yamesemwa leo Agosti 13,2022 jijini Dodoma na Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja,wakati akizungumz na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za mamlaka hiyo na mwelekeo wa utekelezaji wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2022-2023.
Mhandisi Luhemeja, amesema kuwa lengo la mamlaka hiyo ni kuhakikisha upatikanaji maji unafikia asilimia 100 kama ilivyoelekezwa kupitia mpango biashara wa mamlaka hiyo unaotekelezwa kuanzia mwaka 2021/22-2023/24.
Ameitaja miradi hiyo ya kimkakati ni mradi wa uboreshaji mfumo wa usambazaji maji kuanzia Chuo kikuu cha Ardhi hadi Bagamoyo, miradi ya maji Mshikamamo, mradi wa maji Kigamboni, mradi wa maji Chalinze awamu ya tatu, mradi wa ujenzi wa bwawa la Kidunda, miradi ya maji safi pembezoni na mradi wa kupunguza kiwango cha maji yasiyolipiwa.
Miradi mingine ni mradi wa Uboreshaji wa Ufanisi wa Utendaji (PIP), mradi wa ujenzi wa mtambo wa majitaka Mbezi Beach, mradi wa ujenzi wa mtambo wa majitaka Buguruni, mradi wa uboreshaji wa mifumo ya majitaka pembezoni, mradi wa ujenzi wa vituo vya huduma za usafi kwa umma na ununuzi wa magari ya majitaka.
‘Sh. bilioni 388 zimetengwa kwani ujenzi wa bwawa hilo utawezesha kuhifadhi maji lita trilioni 1.6 ambapo tayari sh. bilioni 60 zimetolewa na mkandarasi anatarajiwa kukabidhiwa mradi, Oktoba mwaka huu.’amesema Mhandisi Luhemeja
Mhandisi Luhemeja,ameeleza kuwa mamlaka hiyo inaendelea kuhakikisha wananchi waishio maeneo ya pembezoni mwa Dar es Salaam wanapata huduma ya maji yenye uhakika kwani imetenga sh. bilioni 22 kufanikisha mradi huo.
”Mamlaka hiyo itajenga mtambo mkubwa wa uzalishaji maji katika Mto Rufiji unaotarajiwa kuzalisha lita milioni 750 za maji kwa siku, hivyo kuongeza uhakika wa upatikanaji maji kwa wakazi wa Dar es Salaam na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Pwani.”
Vilevile, amesema sh. bilioni 207 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa mtambo wa kuchakata maji taka eneo la Buguruni ambao awali ulipangwa kujengwa eneo la Jangwani.
Aidha Mhandisi Luhemeja,amesema kuwa hali ya upatikanaji maji, sehemu kubwa ya eneo linalohudumiwa na DAWASA linapata huduma ya maji ya uhakika baada ya miradi ya kimkakati kukamilishwa ikiwemo upanuzi wa mitambo ya Ruvu Juu na Ruvu Chini, ulazaji mabomba na ujenzi wa matenki ya kuhifadhi maji.
”Hii imepelekea idadi ya wateja kuongezeka kutoka wateja 217,766 mwaka 2018 hadi kufikia wateja 370,982 mwaka huu 2022”amesema
Amesema Miradi ya kimkakati ambayo imeanza kutoa huduma kwa wananchi ni pamoja na mradi wa kusambaza maji Makongo hadi Bagamoyo, mradi wa maji Jeti-Buza, mradi wa maji Mkuranga, mradi wa maji Pugu – Gongo la mboto,
Miradi mengine ni mradi wa maji Kibamba – Kisarawe, mradi wa maji Mlandizi – Chalinze – Mboga, mradi wa maji Mbwawa, mradi wa maji Soga, mradi wa maji Tan-choice, mradi wa maji Zegereni na miradi mbalimbali ya uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA ili kuboresha huduma kwa wateja na kupunguza gharama za uendeshaji.
Hata hivyo amesema kuwa baada ya kukamilika kwa utekelezaji wa miradi hii ya majisafi na usafi wa mazingira, kazi itakayobaki itahusisha usogezaji wa huduma kwa wananchi na kufanya maunganisho kwa wateja wapya.