Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Wananchi wa Mkoa wa Iringa alipowasili katika Uwanja wa CCM Samora kwa ajili ya kuhutubia Mkutano wa Hadhara tarehe 12 Agosti, 2022.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Wananchi wa Mkoa wa Iringa kwenye Mkutano wa Hadhara uliofanyika katika Uwanja wa CCM Samora tarehe 12 Agosti, 2022.
************************
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameziagiza Halmashauri za mkoa wa Iringa kutambua maeneo ya malisho na kuyapima ili kupunguza muingiliano wa matumizi ya ardhi na migogoro ya wakulima na wafugaji.
Rais Samia ametoa agizo hilo leo wakati akiwahutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Samora.
Aidha, Rais Samia amewataka wananchi wafuge kwa kufuata kanuni za ufugaji bora na kuendelea kuelimishwa kufuga kibiashara kwa kuzingatia mahitaji ya soko ili kupata manufaa makubwa.
Kwa upande mwingine, Rais Samia amesema Serikali inatambua mchango wa Mkoa wa Iringa katika kilimo kwa nchi, hivyo inachukua hatua anuwai kuhakikisha kuwa wakulima wanapata pembejeo kwa gharama nafuu.
Vile vile, Rais Samia amesema Serikali imeweka ruzuku kwenye mbolea za kupandia na kukuzia ili kupunguza gharama za uzalishaji kwa wakulima.
Serikali imeongeza bajeti ya kilimo kutoka shilingi bilioni 294 mwaka 2021/22 hadi kufikia shilingi bilioni 954 mwaka 2022/23 ili wakulima wazalishe mazao ya kilimo kwa tija na wananchi wote wanufaike na kilimo.