NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi, akizungumza na wanachama na viongozi mbali mbali katika Tawi la CCM Ukunjwi katika ziara yake ya kuimarisha Chama Wilaya ya Wete Pemba.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi,akikabidhi mabati kwa ajili ya kuezekea Ofisi ya Tawi la CCM Shengejuu Pemba.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk. Abdulla Juma Mabodi,akizungumza na Kamati ya siasa ya CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba mara baada ya kuwasili kwa ajili ya ziara yake ya kikazi.(Picha na Is-haka Omar).
………………………………………..
NA IS-HAKA OMAR,PEMBA.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi, amesema hatua kubwa za kimaendeleo zilizofikiwa nchini chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.hussein Ali Mwinyi zinatakiwa kuenziwa na kuthaminiwa.
Kauli hiyo aliitoa katika mwendelezo wa ziara yake ya kikazi ya kuimarisha uhai wa Chama katika maeneo tofauti Wilaya ya Wete Pemba.
Alisema Chama Cha Mapinduzi kinajivunia kutekelezwa kwa ufanisi Ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020/2025 kama kilivyoahidi katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.
Alisema wananchi katika maeneo mbalimbali mijini na vijijini wananufaika na fursa mbalimbali zikiwemo miundombinu bora,huduma za kiafya,elimu,ufugaji kilimo cha kisasa pamoja na mikopo ya masharti nafuu kwa vikundi vya ujasiriamali.
Alifafanua kwamba Rais Dk.Mwinyi ameendelea kuonyesha kwa vitendo dhamira yake ya kuondosha umasikini kupitia falsafa yake ya uchumi wa blue.
“ CCM itaendelea kusimamia vyema sera zake ili wananchi wote wanufaike na fursa mbali mbali za kimaendeleo.”alisema Dk.Mabodi.
Katika maelezo yake Dk.Mabodi, aliwasihi wanachama wa CCM kuendelea kueneza itikadi za Chama ili kuongea wanachama wapya ambao ndio mtaji wa kisiasa wa chama hicho.
Akizungumzia uchaguzi unaoendelea hivi sasa ndani ya chama aliwataka Wana CCM kuendelea kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali ili wapatikane viongozi bora watakaofanikisha ushindi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Pamoja na hayo aliwakumbusha Wana CCM na wananchi kwa ujumla katika wilaya hiyo kujitokeza kuhesabiwa katika zoezi la sensa ya watu na makaazi inayotarajiwa kufanyika Augosti 23,mwaka huu.
Pamoja na hayo aliwataka kuendeleza utamaduni wa kudai risiti za kielektroniki kila wanaponunua bidhaa ili kuchangia ukuaji wa pato la taifa.