Na Mwandishi wetu, Dar
Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemed Mgaza amekutana kwa mazungumzo na Balozi wa Oman nchini Tanzania Mhe. Saud bin Hilal bin Saud Al Shidhan katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Kukutana kwa viongozi hao kumelenga kuendelea kuimarisha masuala mbalimbali ya ushirikiano baina ya Tanzania na Oman pamoja na kufuatilia masuala waliyokubaliana wakuu wa nchi hizo mbili wakati wa ziara ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan nchini Oman mwezi Mei 2022.
Viongozi hao pia wamejadili utekelezaji wa Mkataba wa Makubaliano (MoU) pamoja na mikataba mbalimbali iliyosainiwa na pande hizo mbili. Aidha, mikataba ambayo hadi sasa imesainiwa ni ya ushikiano katika sekta za elimu, uwekezaji, maliasili, pamoja na ushirikiano katika chakula na usalama baina ya Tanzania na Oman.
Pamoja na mambo mengine, viongozi hao wamedajili namna bora ya kutekeleza Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano baina ya Tanzania na Oman (JPC) ili kufungua zaidi maeneo mengine ya ushirikiano.
Balozi wa Oman nchini Tanzania Mhe. Saud bin Hilal bin Saud Al Shidhan akizungumza na Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemed Mgaza (hayupo pichani) katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemed Mgaza akimsikiliza Balozi wa Oman nchini Tanzania Mhe. Saud bin Hilal bin Saud Al Shidhan (hayupo pichani) walipokutana kwa mazungumzo katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemed Mgaza akimueleza jambo Balozi wa Oman nchini Tanzania Mhe. Saud bin Hilal bin Saud Al Shidhan walipokuwa kwa mazungumzo katika ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam