………………………………
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Balozi Fatma Rajab amekutana kwa mazungumzo na ujumbe wa wataalam kutoka Wizara ya Mazingira, Maji na Kilimo ya Saudi Arabia ambao upo nchini kwa ziara ya kikazi kuanzia tarehe 10 -13 Aug,2022.
Ujumbe huo umeambatana na Balozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia, Mhe. Ali Mwadini. Aidha, ziara hiyo ni matokeo ya ziara iliyofanywa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula mwezi Machi 2022 nchini Saudi Arabia ambapo katika ziara hiyo ilikubaliwa kuwa wataalamu hao kufanya ziara nchini Tanzania kwa lengo la kujionea fursa mbalimbali za uwekezaji hapa nchini katika sekta za kilimo na ufugaji.
Pamoja na mambo mengine, wataalam hao wamekutana na wadau kutoka Chemba ya Wafanyabiashara wa Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC), Wizara ya Uchumi wa Buluu, Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Nchini (TAWA), Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) pamoja na Taasisi ya Kuendeleza Kilimo Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini (SAGCOT).
Maeneo mengine ambayo ujumbe huo unatarajiwa kutembelea ni pamoja na kiwanda cha Tanchoice kilichopo Kibaha mkoani Pwani na Ranchi ya Mbogo ili kiujionea fursa za uwekeji katika maeneo hayo.