Na Asteria Muhozya, Steven Nyamiti na Bibiana Ndumbaro – Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo amepongeza ubunifu uliofanywa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa kuanzisha mradi wa mkaa mbadala wa kupikia unaotokana na Makaa ya Mawe.
Amesema kuwa, hatua hiyo ya kuanzisha mkaa mbadala wa kupikia unaotarajiwa kuzinduliwa Agosti 12, 2022 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, matumizi yake yatasaidia kupunguza athari za ukataji miti inayotumika kama nishati ya kupikia kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na kuongeza kwamba, STAMICO imeona mbali.
Waziri Jafo ameyasema hayo Agosti 11, 2022 jijini Dodoma katika eneo la Ipagala wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya upandaji miti wa shirika hilo yenye kaulimbiu isemayo ‘’ STAMICO na Mazingira At 50’’ ikiwa ni kuelekea kilele cha maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake.
Katika hatua nyingine, Waziri Jafo, amelipongeza Shirika hilo kwa kuanzisha kampeni ya utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti ipatayo 540 katika eneo la Ipangala jiijini Dodoma pamoja na maeneo mengine ambayo shirika hilo linatekeleza miradi yake.
Amesema kampeni hiyo inaunga mkono jitihada zinazofanywa na serikali kupitia kampeni mbalimbali za kitaifa za upandaji miti ikiwemo ile ya mwaka 2017 na mwaka 2021 ikiwa ni jitihada za Serikali za kuhifadhi mazingira na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ambayo yameonesha athari kubwa katika baadhi ya maeneo duniani.
‘’Tumeshudia matukio mbalimbali yanayosababishwa na athari za mabadiliko ya tabia nchi duniani ikiwemo kupanda kwa joto katika baadhi ya nchi, kupotea kwa baadhi ya visiwa duniani hivyo, tukio hili la STAMICO kuanzisha kampeni hii ni la kupongezwa,’’ amesisitiza Waziri Jafo.
Kufuatia hatua hiyo, amelitaka shirika hilo kuhakikisha miti hiyo inatunzwa vizuri na kuendelezwa ikiwemo kuwekwa senge’nge na geti maalum katika eneo hilo la Ipangala ambalo miti hiyo imepandwa na kuzitaka taasisi nyingine kuiga mfano wa STAMICO.
Pia, amewataka wakurugenzi wa halmashauri nchini kuhakikisha kwamba wanapogawa viwanja na kutoa vibali vya ujenzi wa makazi wahakikishe ramani za ujenzi zinaonesha maeneo ya upandaji miti ili kuendana na Ajenda ya utunzaji wa mazingira na kuweka mazingira ya kijani.
Naye, Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko akizungumza katika uzinduzi huo, amelitaka shirika hilo kuhakikisha kuwa miti yote elfu mbili (2,000) inayotarajiwa kupandwa katika jiji la Dodoma inaonekana na kukua badala ya kulichukulia tukio hilo kama la kupiga picha tu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amelipongeza shirika hilo kwa kuonesha utashi wa kuifanya Dodoma ya kijani pamoja na kushiriki kikamilifu katika kampeni ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira.
Amesema uchimbaji madini ni miongoni mwa shughuli zinazopelekea uharibifu wa mazingira ikiwa hakuna mpango madhubuti wa kuhifadhi mazingira hivyo, STAMICO kwa kulitambua hilo, imeonesha mfano mzuri kwa kuendeleza mkakati wa serikali kikamilifu na kwa vitendo.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa STAMICO Dkt. Venance Mwasse amesema STAMICO imeipa hadhi ya kipekee kampeni ya kitaifa kwa kuhifadhi uoto wa asili na mazingira ambapo imepanga kupanda jumla ya miti ipatayo elfu kumi (10,000) katika maeneo ambayo inatekeleza miradi yake huku likipanga kupanda miti elfu mbili (2,000) katika meneo yaliyotolewa na mkoa wa Dodoma ambapo kwa kuanzia, imepanda miti 540 katika eneo la Ipagala jijini Dodoma.
Amesisitiza kwamba, shirika hilo litachukua jukumu la kuilinda miti hiyo mpaka pale itakapokuwa na wakati wote kampeni hiyo itaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘’ Panda miti tumia mkaa mbadala wa Rafiki Briquettes’’.
Uzinduzi wa kampeni ya STAMICO na Mazingira At 50’’ umetanguliwa na matembezi ya hisani na mazoezi ya viungo na kuhudhuriwa na washiriki mbalimbali kutoka Wizara ya Madini, taasisi zake, uongozi wa mkoa wa Dodoma, vikundi vya mazingira, mabalozi wa mazingira, wadau wa sekta ya madini na wananchi wanaoishi maeneo ya jirani.