Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga (kulia) akikaribishwa rasmi ofisini kwake jana mjini Sumbawanga na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Joseph Mkirikiti (kushoto).
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga akisalimiana na wajumbe wa Baraza la Amani la mkoa wa Rukwa jana alipowasili rasmi ofisini kwake mjini Sumbawanga.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga akisalimiana na wakuu wa taasisi za umma na binafsi jana wakati wa hafla ya mapokezi rasmi kwenye viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Mkuu wa Wilaya Wilaya ya Kalambo Tano Mwera (kulia) akisalimiana na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga (kushoto) jana mjini Sumbawanga. Katikati ni aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo Joseph Mkirikiti.
………………………….
Na. OMM Rukwa
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Queen Sendiga amesema anatamani kuona mkoa wa Rukwa ukifanya mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo kiwe cha kibiashara na kukuza uchumi wa wananchi.
Ili kufanikisha hilo amewataka wataalam wa kilimo katika halmashauri zote nne za Rukwa kuja na mikakati ya kufanya kilimo kichangie zaidi katika kukuza pato la wananchi na kuongeza uhakika wa chakula.
Mkuu huyo wa Mkoa amesema hayo jana mjini Sumbawanga (10 Agosti, 2022) wakati wa hafla rasmi ya makabidhiano ya ofisi toka kwa mtangulizi wake Joseph Mkirikiti kufuatia Rais Samia Suluhu Hassan kumteua kuwa Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
“Natamani kuiona Rukwa ikifanya mapinduzi makubwa katika kilimo. Maafisa kilimo na ugani jitahidini kuwa na mipango mizuri ili kilimo chetu kiwe cha kibiashara na kuhusisha vijana wengi “alisema Sendiga.
Sendiga aliongeza kusema mkoa lazima uwe na mkakati wa kufanya vijana wengi kurudi vijijini ili kufanya kazi za kilimo hatua itakayowapatia uhakika wa ajira hivyo kutimiza lengo la Rais Samia kutaka kuona kilimo kuzalisha ajira nyingi nchini.
Katika hatua nyingine Sendiga amewaeleza wananchi kuwa atapenda kuona mkoa wa Rukwa ukipiga hatua kubwa katika sekta ya elimu ili watoto wengi zaidi wafaulu mitihani na taaluma kukua zaidi.
Kuhusu usimamizi wa mapato na matumizi ya fedha za umma, Sendiga ametoa rai kwa halmashauri za Rukwa kuziba mianya yote ya upotevu wa mapato ili fedha nyingi zaidi zitumike kutekeleza miradi ya maendeleo.
“Natamani wataalam wa halmashauri waje na mipango madhubuti ya ili tuwe na miradi inayokamilika kwa wakati .Sipendi kuona maboma yasiyokamilika kwenye halmashauri zetu” alisisitiza Sendiga.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa anayemaliza muda wake Joseph Mkirikiti alitumia nafasi hiyo kuwaaga wana Rukwa ambapo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumwamini kipindi alichoongoza mkoa huo.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Rukwa Rainer Lukala akizungumza kwenye hafla hiyo alimpongeza Mkuu wa Mkoa mpya ambapo alimtaka kushirikiana na chama hicho kutekeleza Ilani ya Uchaguzi.
“Tunaamini kazi unayokuja kufanya Mkuu wetu mpya wa Mkoa (Sendiga) ni usimamizi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ili wananchi wa Rukwa wapate maendeleo. Tuko tayari kushirikiana nawe” alisema Lukala.
Lukala aliongeza kusema wanampongeza Mkuu wa Mkoa aliyepita Joseph Mkirikiti kwa ushirikiano wake na chama na kuwa wamepokea mabadiliko yaliyofanywa na Rais vema.
Mkuu wa Mkoa Queen Sendiga anakuwa mkuu wa mkoa wa Rukwa wa 17 tangu ulipoanzishwa mwaka 1974.