Mfanyabiashara maarufu jijini Arusha ,Philemon Mollel(Monaban)akionyesha cheti hicho cha shukrani mara baada ya kukabithiwa na halmashauri hiyo jijini Arusha.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Arusha, Ojung’u Salekwa akimkabithi cheti cha shukrani mfanyabiashara maarufu jijini Arusha,Dk Philemon Mollel jijini Arusha
……………………………………….
Julieth Laizer,Arusha
Arusha.Halmashauri ya Arusha kupitia baraza la madiwani wamemkabithi mfanyabiashara maarufu Dk Philemon Mollel (Monaban) cheti cha shukrani kwa kuchangia mifuko 60 ya saruji kwa ajili ukarabati wa madarasa shule ya sekondari Oldadai katika halmashauri ya Arusha.
Akikabithi cheti hicho leo jijini Arusha katika baraza hilo, Mkurugenzi wa halmashauri ya Arusha ,Suleman Msumi amesema kuwa, wamefikia hatua ya kukabithi cheti hicho kutokana na mchango mkubwa alionao katika shughuli mbalimbali za maendeleo .
Amesema kuwa,walikuwa na zoezi la kitaifa ambalo hufanyika kila mwaka la mwenge wa uhuru kwa ajili ya kuweka jiwe la msingi na kuzindua baadhi ya miradi ya halmashauri hiyo iliyofanyika julai mwaka huu.
“Tuliweza kushirikisha wadau mbalimbali kuhusiana na swala letu ambapo Dk Philemon alifanikiwa kutupatia mifuko 60 ya saruji kwa ajili ya kumalizia shule ya sekondari Oldadai,na hivyo kwa kutambua mchango wake tukaona ni busara kwa halmashauri kumkabithi cheti cha shukrani.”amesema Msumi.
Kwa upande wake,Mfanyabiashara huyo Dk Philemon Mollel ameshukuru sana baraza hilo kwa kutambua mchango wake na kukumbuka fadhila kwa kumkabithi cheti cha shukrani jambo ambalo linatoa motisha wa kuendelea kusaidia zaidi.
Dk.Mollel amesema kuwa,kitendo kilichofanywa na halmashauri hiyo ni jambo kubwa sana na linahitaji kuigwa na taasisi zingine ili watu waendelee kuwa na motisha wa kuisaidia jamii katika maswala mbalimbali.
“Mimi niseme tu nimefurahishwa sana kwa zoezi hili na kipekee naahidi kuendelea kusaidia zaidi katika maswala mbalimbali ya maendeleo ili jamii yetu iweze kusonga mbele na kuondokana na changamoto mbalimbali. “amesema Mollel.