Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masalla akikabidhi jezi kwa nahodha wa timu ya mpira wa miguu kata ya Kayenze
Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masalla akiwa katika picha ya pamoja na manahodha wa timu 20 zitakazoshiriki mashindano ya The Angeline Ilemela Jimbo Cup 2022
Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masalla akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa timu za kata zinazoshiriki mashindano ya The Angeline Ilemela Jimbo Cup 2022
*****************************
Mashindano ya mpira wa miguu ya The Angeline Ilemela Jimbo Cup msimu wa mwaka 2022 ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama cha mapinduzi
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hasan Elias Masalla wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa timu 20 zinazoundwa na kata 19 za manispaa ya Ilemela na timu Moja maalum kutoka mtaa wa kisiwa cha Bezi ambapo amesema kuwa mbali na sekta ya michezo kuwa ni afya na ajira lakini pia ni utekelezaji wa ilani hivyo kumpongeza na kumsifu muandaaji wa mashindano hayo Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula
‘.. Ni wabunge wachache wanaoweza kuanzisha jambo na wakalisimamia, nimekuwa Mbunge ninajua gharama za kuendesha mashindano kama haya, Mashindano haya yana gharama ya muda lakini yana gharama ya kifedha ..’ Alisema
Aidha Mhe Masalla amewataka viongozi na timu zinazoshiriki mashindano hayo kufuata Sheria, taratibu na kanuni za mashindano zilizowekwa Ili kutoa fursa ya ushindani uliosawa kwa wote
Kwa upande wake Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Ilemela Ndugu Kazungu Safari Idebe amefafanua kuwa mshindi wa kwanza wa mashindano hayo atajinyakulia kitita cha shilingi Milioni Mbili, kikombe kimoja, seti Moja ya jezi na mpira wakati mshindi wa pili akibeba kitita cha shilingi Milioni Moja na nusu jezi seti Moja na mpira huku mshindi wa tatu akiondoka na shilingi Milioni Moja, jezi seti Moja na mpira
Bwana Kazungu ameongeza kuwa mchezaji bora atapata kiasi cha shilingi laki Moja, goli kipa bora ataondoka na laki Moja, kocha bora atabeba laki mbili, kikundi bora cha ushangiliaji kitabeba kiasi cha shilingi laki tatu, Msimamizi Bora wa timu Kwa maana ya mtendaji wa kata atabeba laki Moja na mwandishi bora atakaeripoti mashindano hayo ataondoka na kiasi cha shilingi laki mbili hivyo kuwaasa kujipanga vizuri kwaajili ya kushindania zawadi hizo zitakazotolewa na Mbunge Mhe Dkt Angeline Mabula
Nae mratibu wa mashindano hayo ambae pia ni Katibu wa chama Cha mpira wa miguu wilaya ya Ilemela Ndugu Almas amesema kuwa mbali na kuongeza timu zinazoshiriki mashindano hayo kutoka 19 kuwa 20 lakini pia mwaka huu wameongeza kipengele cha kadi badala ya kutoa fomu peke yake kwaajili ya kudhibiti usajili wa mamluki sambamba na kutoa onyo Kwa viongozi wa kisiasa kuacha kuingilia taratibu za mpira na kulazimisha timu zinazotoka katika maeneo yao zitangazwe mshindi au upendeleo wowote sanjari na kupiga marufuku usajili wa wachezaji wa ligi kuu, ligi daraja la kwanza, ligi daraja la pili na ligi daraja la tatu kwakuwa lengo la mashindano hayo ni kuibua vipaji vipya.
Dishoni Moshi ni mchezaji kutoka timu ya kata ya Buswelu na Hassan Hamis ni mchezaji kutoka timu ya kata ya Nyasaka kwa upande wao wamempongeza na kumshukuru Mbunge huyo Kwa kuanzisha mashindano lakini pia kuahidi kufanya vizuri Kwa timu zao kuibuka kidedea wa mashindano hayo