***********************
AFISA wa Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Shabani Shabani amesema kuna umuhimu mkubwa wa wananchi kujitokeza kushiriki zoezi la Sensa linalotarajiwa kufanyika Agosti 23 mwaka huu na kuwataka kuitumia siku hiyo kikamilifu.
Akizungumza kwa nyakati tofauti kama sehemu ya uhamasisha sensa kwa vijana na wananchi, Shabani amesema kushiriki katika zoezi hilo kuna faida mbalimbali nchi ikiwa ni pamoja na kuiwezesha Serikali kupanga mipango yake ya kimaendeleo kutokana na idadi ya wananchi wake.
“Hatuna budi kwa wananchi wote bila kujali itikadi zetu kujitokeza kwa wingi na kushiriki katika sensa hii ya watu na makazi, hii itasaidia Serikali yetu kufahamu idadi kamili ya wananchi wake na hivyo kuweka mipango yake ya kuwahudumia” amesema Shabani
Afisa huyo amesema Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha analiletea Taifa maendeleo hivyo hata hatua yake ya kutaka sensa ifanyike imelenga kumsaidia kufahamu idadi ya wananchi wake ili kupitia Serikali anayoiongoza aweze kuweka mipango mizuri zaidi ya kimaendeleo hivyo ni vyema akaungwa mkono.
“Wengi hufikiria mtu akiwa Rais basi yupo kwenye nafasi ya faida na raha tupu, hivyo kila aina ya madhila anastahili kubeba, Sio kweli! Urais ni kazi ngumu sana, usingizi mchache na tabu nyingi, Tumtie moyo Rais wetu Mhehimiwa Samia Suluhu Hassan Mafanikio yake ni mafanikio yetu wote.” Shabani
Kada huyo wa muda mrefu wa Chama hicho ameongeza kuwa wao kama vijana wenye nguvu na hari, wamejiandaa kikamilifu kushiriki katika sensa hiyo wakiamini kuwa kwa kufanya hivyo kutaiwezesha Serikali kuja na mipango sahihi ya kimaendeleo kwa ajili ya wananchi wake
Aidha amesema muda tangu Rais Samia aingie madarakani na kuiongoza Serikali ya awamu ya sita ameonyesha dira katika masuala mbalimbali ya kiuchumi na kimaendeleo hali iliyosaidia kuongeza idadi ya wawekezaji kuja kuwekeza nchini.
“Leo hii tunaona kwa macho yetu namna idadi kubwa ya watalii wanaoingia nchini, hili limetokana na wazo lake la kuja na filamu ya Royal Tour ambayo kimsingi imeongeza chachu ya watalii kutoka mataifa mbalimbali kuja kuitembelea Tanzania” amesema Afisa huyo wa CCM
Amesema ujio wa watalii hai mbali na kuliingizia Taifa fedha za kigeni pia utawafanya waone fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini na kwenda kuzitangaza katika mataifa wanayotoka jambo ambalo litazidi kuineemesha nchi.