Baadhi ya akinamama wakiwa na watoto wao wakisherehekea Maadimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji Duniani yaliyofanyika Kitaifa katika wilaya ya Ikungi mkoani Singida hivi karibuni.
******************
Na Abby Nkungu, Singida
SERIKALI imeahidi kuendelea kutenga fedha zaidi na kusimamia utekelezaji wa
miongozo, kanuni na sheria juu ya unyonyeshaji wa watoto maziwa ya mama ili
kulinda afya na ustawi wa kundi hilo
katika jamii.
Kauli hiyo ilitolewa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wanawake na Makundi maalum, Mwanaidi Ali Khamis wakati akizungumza kwenye uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya
unyonyeshaji Duniani yanayofanyika
Kitaifa katika halmsahuri ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida.
Naibu Waziri huyo alisema kuwa lengo la hatua hiyo ya Serikali ni
kuhakikisha watoto wote wananyonyeshwa maziwa ya mama kwa kipindi cha miaka
miwili au zaidi na kutochanganyiwa chakula chochote ndani ya miezi sita ya
awali kama inavyoshauriwa na wataalamu ili kulinda afya zao.
“Hivi sasa ni asilimia 43 tu ya watoto ndio wanaonyonyeshwa hadi kipindi cha miaka miwili na kuendelea
huku takwimu zikionesha asilimia 57 tu ya watoto ndiyo hunyonyeshwa
maziwa ya mama pekee bila kuchanganyiwa na chakula kingine chochote wala
kunyweshwa maji kwa kipindi cha miezi sita” alisema.
Kutokana na hali hiyo alisema pamoja na kutenga fedha, Serikali itaendelea
kusimamia utekelezaji wa sheria, kanuni na miongozo juu ya umuhimu wa akinamama
wanaojifungua kunyonyesha watoto wao kwa kipindi cha miaka miwili au zaidi na
kunyonyeshwa ziwa pekee bila kuwachanganyia na chakula wala maji kwa miezi sita
ili kujenga msingi imara wa afya na uhai wa mtoto.
“Unyonyeshaji watoto maziwa ya mama huzuia aina zote za utapiamlo na
kuwepo uhakika wa chakula kwa watoto wachanga na wadogo” alisema na
kuongeza;
Unyonyeshaji maziwa ya mama ni msingi wa maisha; hivyo kulinda, kuendeleza
na kuimarisha unyonyeshaji wa maziwa ya mama kwa mtoto ni jambo lenye umuhimu
katika kujenga Dunia na Tanzania endelevu”.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Lishe nchini, Dk Germana Leyna
alibainisha kuwa upo uwezekano wa kuepuka unene na uzito usiofaa kwa asilimia
25 pindi mtoto anapokuwa mtu mzima iwapo mama atakuwa amemnyonyesha kikamilifu
na kwa kuzingatia sheria, kanuni na miongozo.
Nao wadau wengine wa masuala ya afya na lishe, wanasema kuwa kauli hiyo juu
ya kusimamia unyonyeshaji imekuja muda muafaka wakati wa utekelezaji wa
Programu Juimuishi ya Taifa juu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya
Mtoto iliyoanza mwaka 2021 na kuendelea hadi mwaka 2025.
“Kikubwa ni wadau kuendelea kushirikiana chini ya Programu hii
inayoshughulika na masuala mtambuka ya watoto kuanzia umri wa miaka 0 hadi 8
ili kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu
wa unyonyeshaji watoto wa maziwa ya mama”alisema Afisa Lishe katika halmashauri
ya Wilaya ya Ikungi Agness John na kuongeza kuwa;
“Hivi sasa kuna mtindo wa baadhi ya akinababa kunyonya maziwa ya mama
badala ya kumwachia mtoto eti wakidai kuwa hiyo ni dawa ya kutoa
“hangover” ya pombe suala ambalo alisema linapaswa kukemewa na
kupigwa vita kwa nguvu zote kwani linamnyima haki mtoto” alisema na
kuungwa mkono na Muuguzi Mkuu Mkoa wa Singida Yasinta Alute ambaye alisema
suala la wanaume kunyonya maziwa ya mtoto limeanza kuota mizizi na linapaswa
kukomeshwa mara moja.
“Sio suala la kumaliza maziwa ya mtoto tu lakini pia lazima utambue kuwa
mtu mzima anaweza kuwa na maradhi na huenda ziwa hata halisafishwi na mtoto
akija kunyonya ziwa hilo hilo, huoni kama kuna hatari ya kumwambukiza mtoto
maradhi?…. akina baba acheni hizo” alisema kwa msisitizo.
Maadhimisho ya Wiki ya unyonyeshaji Duniani ni utekelezaji wa Azimio la
Innocent, Italia la mwaka 1991 ambapo mwaka huu yameongozwa na Kauli mbiu
inasemayo “Chukua hatua, endeleza unyonyeshaji: Elimisha na toa Msaada”
lengo likiwa ni kulinda, kuhimiza na kuendeleza unyonyeshaji watoto maziwa ya
mama kwa ajili ya afya na ustawi wa kundi hilo muhimu.