MKUU wa Mkoa Dodoma, Rosemary Senyamule, akizungumza leo Agosti 10,2022 na Viongozi wa CCM wakati akijitambulisha katika Ofisi za CCM Mkoa wa Dodoma.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Godwin Mkanwa,akizungumza mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, kwenda kujitambulisha katika Ofisi za CCM Mkoa wa Dodoma.
Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pili Mbanga, akizungumza mara baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule, kwenda kujitambulisha katika Ofisi za CCM Mkoa wa Dodoma.
………………………………
Na Odilo Bolgas-DODOMA
MKUU wa Mkoa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema atashirikiana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuhakikisha wanaijenga Dodoma katika Sura ya Kimataifa kwa kuwainua zaidi wananchi katika kuwaletea maendeleo kama ambavyo Ilani ya Uchaguzi ya CCM ilivyoahidi.
Hayo ameyasema leo Agosti 10,2022 jijini Dodoma wakati akijitambulisha katika Ofisi za CCM Mkoa wa Dodoma, Senyamule amesema kuwa miongoni mwa kipaumbele chake ni kuhakikisha kilimo kinakuwa nyenzo muhimu kuwawezesha wananchi kunufaika kiuchumi.
“Asilimia 70 ya wananchi wa Dodoma wanategemea kilimo, Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imeanza kutoa ruzuko za pembejeo za kilimo kwa wakulima kwa lengo la kuboresha uzalishaji. Nitahakikisha ruzuku hizo zinawafikiwa wakulima kwa wakati,”amesema
Amesema kuwa Rais Samia amedhamiria kuinua kilimo cha umwagiliaji mkoani hapa ambapo ameanza kutoa fedha kutekeleza mradi wa umwagiliaji katika wilaya za Chamwino na Bahi.
”Katika Wilaya ya Chamwino, serikali imetoa fedha kuanzisha miradi miwili ya umwagiliaji katika shamba lenye ekari 11,000 huku lingine likiwa na ukubwa wa ekari 8,000 ambayo yatawekewa miundombinu muhimu ya umwagiliaji.”ameeleza
Hata hivyo amesema kuwa sekta ya elimu, bado kiwango cha elimu sio cha kuridhisha hivyo atahakikisha hali hiyo inatatuliwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, Godwin Mkanwa, amesema kuwa Dodoma bado kuna changamoto zinazonahitaji ufumbuzi hususan suala la umasikini.
Awali Katibu wa CCM Mkoa wa Dodoma, Pili Mbanga, amesema wamejipanga kutembelea wilaya za mkoa huo kuhamasisha Sensa ya Watu na Makazi lengo ni kuunga mkono jitihada za Rais Samia za kupata takwimu sahihi kwa ajili ya mipango mbalimbali ya serikali.