*********************
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakari Kunenge amekutana na uongozi wa Shirika la Maendelo la Taifa – NDC kwa mazungumzo ya kuitangaza Kongani ya Viwanda inayomilikiwa na Shirika hilo ,Mjini Kibaha na kuhakikisha inaandaa mchoro wa eneo hilo kwa ajili wawekezaji.
Mazungumzo hayo yalifanyika kwenye ofisi za Mkuu wa Mkoa huo ambapo Kunenge amemshauri Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Nicolaus Shombe kuhakikisha ofisi yake inaandaa mchoro huo ili kuinua uwekezaji.
“Ni wajibu wangu kuzisemea taasisi zote zilizopo mkoani kwangu, hivyo mnapaswa kuandaa mchoro wa eneo hilo, mnipatie ili tuweze kulitangaza kwa wawekezaji wanaotafuta maeneo ya uwekezaji,” alisema Kunenge.
Akifafanua faida za uwekezaji, Kunenge ameeleza kuwa unasaidia katika kufanisha malengo ya mkakati mkubwa wa mkoa wa kuongeza vyanzo vya mapato, hivyo eneo hilo la NDC ni muhimu na litasaidia kuongeza mapato.
Katika Hatua nyingine, amewapongeza watendaji wote wa Sekretarieti ya Mkoa na wa Halmashauri zote za Mkoa wa Pwani kwa utendaji wa kazi na kupelekea mkoa kushika nafasi ya tatu nchini kwa kigezo cha makusanyo yanayotokana na mapato ya ndani.
Nae Mkurugenzi Mtendaji Wa shirika la Maendeleo ya Taifa NDC Dr. Nicolaus Shombe alifafanua kuwa Kongane la Viwanda TAMCO, Kibaha lina eneo ukubwa wa ekari 201.63 na limeteuliwa kujenga Viwanda katika Makundi matatu aliyoyataja kuwa ni Viwanda vya madawa na vifaa tiba, viwanda vya kuunganisha magari na mitambo pamoja na viwanda vya nguo.
Alisema eneo hilo linahitaji miundombinu ya barabara kama kilomita 4.8 na tayari Kilomita 1.6 imeshajengwa.
Dr. Shombe alieleza ,tayari eneo hilo limepelekewa umeme wa Kv 33 na TANESCO huku miundombinu ya maji ikiwa inaendelea kuboreshwa.