Asila Twaha, Tabora
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Elimu) Dkt. Charles Msonde amesema, Mashindano Umoja wa Michezo wa Shule za Sekondari Tanzania(UMISETA) yameanza leo kwa kuzingatia taratibu zote za michezo zinavyotaka.
Akifafanua jumla ya washiriki 3,497 wanamichezo, walimu pamoja na viongozi wao 703 kuwa na jumla ya 4,200 kwa Tanzania Bara na Zanzibar wote wamefika kwa ajili ya michezo hiyo.
Dkt. Msonde amesema, hayo leo Agosti 10, 2022 ikiwa ni muendelezo wa michezo ikiwa leo ni ufunguzi wa michezo kwa shule za Sekondari (UMISETA) katika viwanja vya Tabora Boys Jijini Tabora .
Amsema, kuisha kwa michezo ya Shule za Msingi (UMITASHUMTA) imetoa nafasi kwa kuendelea kwa Shule za Sekondari (UMISETA ) wote wakiwa na haki ya ushiriki wa michezo hiyo.
“Utaratibu wetu katika nidhamu na maadili upo palepale katika kufuata sheria za michezo sababu michezo ni somo, mazoezi lakini pia kujenga mahusiano mazuri” Dkt. Msonde
Awali akisoma hotuba Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Francis Michael amesema, pamoja na michezo hiyo kuendelea wamepokea baadhi ya changamoto ambazo Wizara itazifanyia kazi ikiwemo kucheza kwa wanafunzi wa madasa ya MEMKWA ambao wanaonekana wapo katika umri mkubwa.
“Wizara ya Elimu, kama watunga Sera, Miongozo ya Elimu tutahakikisha tunalishughulikia hili na kuyatekeleza maelekezo yote ya Mhe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyotuelekeza katika ufunguzi wa michezo na vyuo vya ualimu vifundishe na somo la michezo”
Aidha, Dkt. Michael amesema, katika kulipa kipaumbele somo la michezo chuo cha Tabora na Mpwapwa litaongezewa somo la michezo kufanya jumla ya vyuo 6 vinavyofundisha somo la michezo na kutoa walimu wa michezo.
Kwa upande wa Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tabora Bw. Musa Chaulo ametoa wito kwa wanamichezo na wasimamizi wa michezo kujiepusha na vitendo vya utoaji wa rushwa katika michezo ili watakaoshinda washinde kwa haki.