Adeladius Makwega-DODOMA
Agosti 6, 2022 niliandika matini juu ya Mamlaka ya Vitambulisho vya TaIfa (NIDA), mara baada ya matini hiyo kutoka nilipokea maoni mengi ya wadau kadhaa. Kabla sijaanza kuyaweka hapa maoni hayo naomba msomaji wangu fahamu kuwa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) ipo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchi ambayo inaongozwa na Waziri wetu mheshimiwa sana mhandisi Hamad Yusuf Masauni, mbunge wa jimbo la Kikwajuni huko Zanzibar.
Kwa wale ambao hawamfahamu ndugu huyu, kuna wakati aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa, binafsi nilimfahamu muungwani huyu akiwa mwenyekiti wa UVCCM taifa katika baadhi ya vikao vya umoja huo.Ninasema wazi mhesmiwa huyu ni mtu mwema, mtu mstaarabu, mkarimu na anayesikiliza watu sana tangu akiwa UVCCM.
Msomaji wangu kwa sasa naomba nirudi katika maoni niliyoyapokea kutoka kwako.
“Inawezekana kama hii tekinolojia haitusaidii kitu, ukijumlisha na tabia za watu wenyewe kwenye hizi ofisi, siku hizi ni changamoto sana.”
Msomaji wangu wa kwanza aliinua sauti katika hilo.
“Nilienda kujiandiksha Handeni, mkoani Tanga mwaka 2019, namba ya NIDA nilipewa 2020 lakini kitambulisho (ID) mpaka leo sijakipata.”
Msomaji wangu mwingine aliibua hoja hiyo.
“Hivyo vitambulisho vya taifa ni mtihani mkubwa, binafsi nimejiandikisha 2019 nikapewa namba baadaye, kitambulisho sijapata na miaka inasonga.”
Maoni mengine niliyoyapokea yalikuwa hayo,
“Jambo hili ni shida kubwa, watu wengi wamesajiliana namba za simu kutokana na usumbufu wa kupata kadi za NIDA wakati jambo hilo ni kosa kisheria.”
Ndugu huyu mkazi wa Mbagala aliupigilia msumari wa mwisho wa jeneza la maoni huku nikiyaweka kando maoni mengi mezani kwangu.
Baadhi ya wafuatiliaji wa mambo wanadai kuwa mchakato wa kutolewa kitambualisho ni mrefu mno ambao unapitia hatua mbalimbali, kazi hiyo siyo tu ya mtu akishajaza fomu na kupigwa picha, ati hapo kazi imekamilika, hapo michakato ya ndani bado unaendelea.
“Watu ni wengi sana, kuliko uwezo wa mashine inayochapisha nakala za vitambuslisho hivyo, huku ikiaminika kuwa mashine ya kuchapisha ipo moja katika eneo la Kibaha mkoani Pwani.”
Kulingana na hoja hii kunaibuka hoja nyingine, je kwa nini vitambulisho vyote vichapishwe sehemu moja? Hapa la kushauri kwa mheshimiwa Masauni ni kwamba, ni vizuri mashine hizo kuongezwa na kuwepo na vituo vitano vikigawanyika katika kanda, Kanda ya Mashariki, Kanda ya Magharibi, Kanda ya Kaskazini, Kanda ya Kusini na Kanda ya Kati.
Maeneo hayo yote matano pakiwepo na printers itasaidia mno kuokoa na kupunguza malalamiko ya watu na vitambulihso vitapatikana kwa haraka.
“Oh unajua mashine hizo ni gharama kubwa sana zaidi ya mabilioni.” Inawezekana mashine hizo kuuzwa kwa gharama kubwa, lakini gharama kubwa kwa kununua mtu binafsi siyo kwa serikali, serikali inaweza kuzinunua kabisa. Kwa hiyo mheshimiwa Masauni ninashauri ununuzi huo hauna budi kufanyika haraka kabisa.
Kumekuwa na hoja kuwa mshine hizo zinaendesha na wageni ambao wanafanya kazi hapo Kibaha, nadhani hoja hii inatakiwa kufanywa kazi, hata kama upo mkataba ulioingiwa na kampuni hii inayochapisha kadi hizi, kwa sasa ni wakati sahihi wa kufikria vinginevyo na vijana wa Kitanzania wapate mafunzo haraka, mashine zikiweka wao wafanye kazi hiyo.
“Unajua inawezekana gharama ya kuzifanyia ukarabati ni kubwa, kwa hiyo ndiyo maana kazi hiyo wanaifanya hao.”
Haya ni mawazo tu, lakini hata kama gharama ziwe kubwa kiasi gani, nina hakika serikali kwa kuwatumia wataalamu wetu waliopata mafunzo, jambo hili haliwezi kushindikana.
Kumekuwa na hoja kuwa kwetu sisi Watanzania, wakati mamlaka hii ilipokuwa inaanza kazi yake muitikio wetu ulikuwa mdogo, watu wengi wamekuwa wakikimbilia mamlaka hii mara baada ya kuwa na uhitaji wa kadi hiyo, wengine wakisema kuwa wakati huo NIDA walikuwa wakifanya kazi vizuri sana.
“Kuwa na kitambulisho cha NIDA ni muhimu, kiwe kibindoni tu, siku kikihitajika kichukue nenda nacho pale kinapotakiwa.”
Watu wengi wanakwenda NIDA kwa msimu, wakitaka kujiunga na vyuo, masuala ya kusajili kaya masikini au barabara inapitishwa jirani na kiwanja chake . Kwa hoja hii ni kweli Watanzania tunatakiwa kuwa waitikiaji wa mambo kwa haraka sana pale serikali inapoaanzisha jambo, kuepuka usumbufu wa baadaye.
Kwa kuitimisha mheshimiwa Masauni ni vizuri kumuagiza mkurugenzi wa NIDA wasasa ajitahidi mno kuwapatia posho za saa za ziada watumishi wake wote wanaofanya kazi katika ofisi zake wilayani, siyo zile za Dar e Salaam tu.
Kwa utafiti mdogo niliyoufanya unaonesha kuwa ofisi nyingi za NIDA wilayani zinafungwa saa 9.30 alasiri na hata kama kukiwa na wateja waliobaki katika foleni wanaambiwa kuwa warudi ofisini hapo kesho yake. Kitendo hicho kinaweza kustajabisha wengi mno, lakini hilo ndivyo lilivyo. Kama posho za ziada zitalipwa, kazi katika ofisi hizo zitafanyika hadi jioni na hilo litapunguza malalamiko mno kwa mamlaka hii.
Pia mheshimiwa Masauni amwambie Mkurugenzi wa NIDA awe jirani na jamii inayohitaji vitambulisho hivyo, achague hata siku moja awe katika wilaya zenye msongamano mkubwa wa waombaji ashiriki zoezi hilo awasikie Watanzania wanayoyasema dhidi ya taasisi hii.
Waziri Hamadi Masauni, kwa heshima zote jambo hili ninaliweka katika meza yako kusaidia kupatikana kwa kitambulisho hicho angalau saa 24 tu baada ya kujaza fomu.
Mheshimiwa Masauni kwa kufanya hivyo utakumbukwa mno, tutasema;
“Mheshimiwa Hamad Yusuf Masauni ndiye aliyesaidia mno Watanzania kupatikana kwa kadi ya NIDA kwa muda mchache.”