Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na baadhi ya washirki wa Mkutano Mkuu wa 44 wa Shirkisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Cha Arusha (AICC), Agosti 10, 2022. Wa nne kushoto ni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohammed Mchengerwa na wa tatu kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongela.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiongozana na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) Dkt. Patrice Motsepe (kulia) na Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo , Mohammed Mchengerwa (kushoto) wakati alipoingia Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha, ( AICC) kufungua Mkutano Mkuu wa 44 wa CAF, Agosti 10, 2022. Wa Pili kulia ni Rais wa Shirkikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianniu Infantino.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishiriki kuimba Wimbo wa Taifa kabla ya kufungua Mkutano Mkuu wa 44 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), Agosti 10, 2022. Kushoto ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani, Gianniu Infantino na wa watatu kushoto ni Rais wa Shirkikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF), Patrice Motsepe.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofungua Mkutano Mkuu wa 44 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC),
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea zawadi ya nembo ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) kutoka kwa Rais wa Shirikisho hilo, Dkt. Patrice Motsepe baada ya kufungua Mkutano Mkuu wa 44 wa CAF kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC)
Baadhi ya washiriki wa Mkutano Mkuu wa 44 wa Shirkikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF) wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua mkutano huo kwenye Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC).
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
…………………………
MHESHIMIWA Rais Samia Suluhu Hassan amesema Bara la Afrika linahitaji kuongeza juhudi zaidi kwa kuongeza jitihada mbalimbali zitakazoendeleza mpira wa miguu.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Agosti 10, 2022 alipomuwakilisha Mheshimiwa Rais Samia katika ufunguzi wa Mkutano wa 44 wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) jijini Arusha.
“Rais Samia aliamua na kukubali kuwa mdhamini wa mashindano ya Klabu Bingwa kwa vilabu vya Nchi za Afrika Mashariki na Kati (SAMIA CUP) ili kuunga mkono maendeleo ya mpira wa miguu Afrika na duniani.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema Rais Samia anaamini mkutano huo utafungua njia kwa Tanzania kuwa mwenyeji wa mikutano mingine ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) na CAF na kutoa fursa ya kuandaa mashindano mbalimbali yanayoandaliwa na CAF na hata FIFA.
Amesema kuwa kwa miongo kadhaa Tanzania kupitia Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) imekuwa na mahusiano mazuri na CAF pamoja na FIFA. “Mahusino hayo yamekuwa chachu ya kuhamasisha na kuimarisha maendeleo ya mpira wa miguu nchini na ukanda mzima wa Afrika Mashariki.”
“Ujenzi wa vituo viwili vya michezo chini ya TFF kwenye miji ya Tanga na Dar es Salaam ni kielelezo cha mahusiano hayo mazuri. Tunawashukuru sana FIFA kwa uwekezaji huo na kuendelea kutuunga mkono katika kuboresha mchezo huu unaopendwa na watu wengi nchini na duniani kwa ujumla”
Waziri Mkuu amesema ni matarajio ya Tanzania kuwa FIFA itaendelea kubuni miradi mingi zaidi kwa ajili ya kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu kwa nchi zinazoendelea kama Tanzania ambazo zimekuwa zikikabiliwa na changamoto ya ujenzi wa miundombinu ya michezo. “Tanzania kwa upande wake ipo tayari kuendelea kuimarisha uhusiano wake na FIFA na wanachama wake na CAF ikiwemo”
Naye, Rais FIFA, Gianni Infantino amesema kuwa wataendelea kulinda timu za taifa kwa kuwa ni muhimu katika kukuza mpira wa miguu duniani. “Wachezaji wanafuraha kuchezea timu za taifa na hata mataifa yanayo furaha kuona wachezaji wao wanawakilisha timu zao za taifa, FIFA pia tutaendelea kuwekeza na kuhakikisha soka la Afrika lina kua zaidi.”
Amesema kuwa Mwaka 2022 ni mwaka ambao dunia itaungana katika kusherehekea michuano ya Kombe la Dunia nchini Qatar baada ya kupitia kipindi cha ugonjwa wa UVIKO 19. “Tunaamini ni mwaka ambao moja ya nchi ya Afrika inaweza kubeba kombe la dunia”
Kwa upande wake, Rais CAF Dkt. Patrice Motsepe amesema watu wa Afrika wanapenda mpira wa miguu kwa kuwa ni sehemu ya furaha kwa waafrika wengi na anaamini shirikisho hilo litafanikiwa kuhakikisha soka la Afrika linakuwa na ushindani duniani. “Afrika ni moja ya bara ambalo limezalisha wachezaji wengi wanaofanya vizuri duniani.”
Awali, Rais wa TFF, Wallace Karia alisema kuwa wanashukuru kwa mchango mkubwa unaotolewa na CAF na FIFA katika kukuza mchezo wa mpira wa miguu nchini, Afrika na Duniani kwa ujumla.