Wanafunzi waliosoma nje ya nchi kwa mwamvuli wa Global Education Link (GEL), wakifanya usajili na kuchukua majoho kwaajili ya mahafali yao yanayotarjiwa kufanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa Global Education Link (GEL), Abdulmalik Mollel, akizungumza na wanafunzi waliosoma nje ya nchi ikiwa ni siku chache kabla ya mahafali yao yanayotarajiwa kufanyika ukumbi wa Mlimani City Dar es Salaam hivi karibuni.
Wanafunzi waliosoma nje ya nchi kwa mwamvuli wa Global Education Link (GEL), wakimsikiliza Mkurugenzi wa GEL, Abdulmalik Mollel wakati wa mafunzo kabla ya mahafali yao yanayotarajiwa kufanyika hivi karibuni kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam
*************************
Na Mwandishi Wetu
SECRETARIETI ya Ajira, imesema moja ya chngamoyo inayosababisha vijana wengi kukosa ajira ni kushindwa kujiandaa vizuri kabla ya kwenda kwenye usaili wa kazi.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu wa Sekretarieti ya Ajira anayesimamia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Samwel Tanguye, wakati akizungumza na wanafunzi waliosoma nje ya nchi.
Wanafunzi zaidi ya 400 waliosoma nje ya nchi kwa mwamvuli wa Global Education Link (GEL), wanatarajiwa kushiriki mahafali yao kwenye ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Alisema wanapoitwa kwenye usaili wa kazi wanapaswa kujiandaa vya kutosha kwa kuhakikisha wanamudu kujibu maswali yote watakayoulizwa badala ya kukurupuka.
“Mfano umeitwa kwenye usaili wa udaktari hata kama umemaliza leo kuna mambo mengi unapaswa kujikumbusha kabla ya kwenda kwenye mahojiano, kwa hiyo unapaswa kuendelea kujifunza ili ukiulizwa jambo kwenye taaluma yako uwe vizuri,”
Alisema vijana wengi wamekuwa wakidhani kwamba ajira zinatolewa kwa upendeleo jambo ambalo si kweli kwani zimekuwa zikitangazwa kwa uwazi na usaili unafanywa kwa haki kwa kila anayewasilisha maombi.
Alisema mara kadhaa sekretarieti hiyo inapoitisha usaili mkoani Dodoma vijana wengi wa Dar es Salaam wamekuwa hawaendi kwa visingizio vya kukosa nauli.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni vijana wengi kushindwa kusoma vizuri matangazo ya ajira hivyo kujaza fomu za maombi ambazo hazijakamilika hali inayosabisha malalamiko kwamba ajira ni za upendeleo.
“Mfano umeambiwa ambatanisha cheti kilichothibitishwa na mwanasheria wewe unachukua cheti chako tu unatuma hivyo hivyo bila kupeleka kwa mwanasheria unatarajia nini wakati umeshindwa kufuata maelekezo,” alisema
Alitaja changamoto nyingine ya vijana kukosa kazi kwamba ni kupeleka maombi ya kazi sehemu isiyohusika jambo linalosababishwa na kukosa utulivu wakati wa kusoma matangazo ya ajira.
“Unakuta nafasi za kazi zimetoka TRA lakini aliyetangaza nafasi hizo ni Sekretarieti ya Ajira sasa unakuta mhitimu anajaza mambo yake vizuri lakini badala ya kutuma maombi yake kwa sekretarieti iliyotangaza kazi yeye anatuma maombi hayo TRA,” alisema
Alisema mara baada ya kuhitimu wanatakiwa kupeleka vyeti vyao Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), ambayo ndiyo yenye mamlaka ya kuthibitisha uhalali wa cheti kwa kupatia mhusika uthibitisho.
Alisema ni kweli serikali imekuwa mwajiri mkuu lakini hata hivyo haiwezi kuajiri watanzania wote hivyo wengine wanaweza kutumia ujuzi walioupata kujiajiri na kuajiri wenzao.
“Yapo mataifa kama China vijana wao wanauza ujuzi wao nyinyi tayari mnaujuzi msikae vijiweni kulalamika tumieni ujuzi wenu kutazama fursa zilizopo Afrika Mashariki, Afrika, Ulaya na hata Marekani,” alisema.
Alisema milango ya uwekezaji imefunguliwa na wawekezaji wamekuwa wakimiminika kuwekeza kwenye miradi mbalimbali hivyo vijana wanapaswa kujiandaa kuchangamkia fursa za kufanyakazi kwenye makampuni hayo.
Alisema vijana wengi wanaposoma wanapata ulemavu wa fikra kwamba ni lazima afanyie kazi taaluma aliyosomea hata kama anaona fursa kwenye eneo lingine zitakazomwingizia fedha nyingi.
“Unakuta msomimzuri wa utawala wa biashara anasubiri aajiriwe ofisini, anakaa nyumbani mwaka ukimwuliza vipi anakwambia kazi hazijatoka wakati ameungukwa na fursa nyingi sana,” alisema
Aidha, alisema vijana waliosoma nje ya nchi wameona mambo mengi mazuri wanayoweza kufanya na kuwaingizia kipato tofauti na ambao hawakupata fursa hiyo.
“Nyinyi mnapaswa mtengeneze fursa za ajira kwa wengine kwasababu vichwa vyenu vimejaa ujuzi mwingi na mmeona fursa nyingi huko mlikotoka. Kukariri kwamba umesomea kitu flani na huwezi kufanya biashara nyingine huo ni ulemavu,” alisema
Aliwapongeza wanafunzi hao kwa kufanikiwa kuhitimu shahada zao nje ya nchi na kwamba anamatumaini makubwa wamepata ujuzi ambao watautumia kwaajili ya manufaa ya kundeleza taifa lao.