MKURUGENZI Mtendaji Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jiji la Arusha (AUWSA) Mhandisi Justine Rujomba,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Agosti 10,2022 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa shughuli za Mamlaka hiyo na Mwelekeo wa utekelezaji wa mwaka wa fedha 2022/23.
………………………………..
Na Alex Sonna-DODOMA
KATIKA Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2022/23,Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira jiji la Arusha (AUWSA) imepanga kutekeleza miradi itakayogharimu shilingi bilioni 11.8 ili kuongeza hali ya upatikanaji wa huduma ya maji katika jiji hilo.
Hayo yamesemwa leo Agosti 10,2022 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira jiji la Arusha (AUWSA) Mhandisi Justine Rujomba,wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za Mamlaka hiyo na Mwelekeo wa utekelezaji wa mwaka wa fedha 2022/23.
Mhandisi Rujomba amesema Mamlaka hiyo imepanga kutekeleza miradi inayogharimu shilingi bilioni 11.8 ya fedha za ndani za Mamlaka ili kuongeza hali ya upatikanaji wa huduma katika eneo lake.
” AUWSA itajenga mtandao mpya wa majisafi kwa urefu wa kilomita 215.961 katika maeneo mbalimbali,itaunganisha wateja wapya 13,993 kati ya hao wateja 10,893 katika Jiji la Arusha, na wateja 3,100 miji midogo,kuongeza mtandao wa majitaka kwa kilomita 10 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha,Kuunganisha wateja 4,200 katika huduma ya uondoaji wa majitaka,”amesema Mhandisi Rujomba
Hata hivyo Mh.Rujomba amesema Mamlaka hiyo itajenga chemba za kuhifadhia dira za wateja dhidi ya uharibifu na wizi wa dira za maji, ambapo chemba 1,237 zinajengwa ili kuhamishia dira 5000 za wateja wa majumbani.
“Kumekua na changamoto ya wizi wa maji hadi sasa zaidi ya watu 55 wamekamatwa kwajili ya wizi wa maji na tukiwakamata tunakaa nao chini tunawaelekeza juu ya utunzaji miundombinu ya maji baada ya hapo wanalipa faini na hadi kufikia sasa waliokamatwa wamelipa faini ya shilingi milioni 65 za Tanzania,”amesema.
Aidha amesema kuwa Mamlaka imeendelea kupanua huduma baada ya kuongezewa maeneo ya kutoa huduma ikiwamo kata saba za Wilaya ya Arumeru, pamoja na miji midogo ya Longido, Monduli, Ngaramtoni na Usa River.
“Mahitaji halisi ya maji kwa sasa ni lita milioni 124.7 kwa siku kwa mchanganuo ambapo Jiji la Arusha mahitaji lita milioni 109.6 huku miji midogo mahitaji yakiwa lita milioni 15.09,”amesema.
Aidha amesema Maji yanayozalishwa kwasasa ni lita Milioni 84.5 kwa siku kutoka kwenye vyanzo vya visima virefu, chemchem na mito sawa na asilimia 68 ya mahitaji. huku matarajio ni kufikia asilimia 95 ya upatikanaji wa maji mijini kulingana na lengo lililowekwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kabla ya kufika mwaka 2025.
“Kabla ya uwekezaji wa Serikali kupitia utekelezaji wa mradi mkubwa, uzalishaji wa maji ulikua ni wastani wa lita Milioni 40 kwa siku na huduma ya uondoaji wa majitaka ilikua ni wastani wa asilimia 7.6 ya wakazi wa Jiji la Arusha ambapo kwa sasa kiwango cha uzalishaji maji kimeongezeka kwa lita Milioni 26 kwa siku,
“Ongezeko hilo limewezesha kuboresha upatikanaji wa maji kwenye maeneo yaliyokuwa na uhaba wa maji hasa katika maeneo ya Moshono, Kiserian, Murrieti, Olasiti, Sombetini, Kwa Moromboo, Olmoti, Sokoni 1, na baadhi ya maeneo ya Terati na kuchangia kuongeza saa za huduma kutoka masaa 15 hadi 19 kwa siku.
Pia amesema kuwa AUWSA imewataka wananchi wa Arusha kuendelea kutunza miundombinu ya maji pamoja na vyanzo vyake ili kurahisisha upatikanaji wa huduma bora za maji.