Afisa Ustawi wa Jamii manispaa ya Ilemela Bi Stella Mbura akimkabidhi sare za shule zilizotolewa na shirika la MOCSO mwanafunzi wa shule ya msingi Gedeli iliyopo kata ya Nyakato
Picha ya pamoja ya wanafunzi walionufaika na sare za shule zilizotolewa na shirika la MOCSO
Mratibu wa afya shuleni wa manispaa ya Ilemela Bwana Finias Nyaganyi akizungumza na watoto na wazazi waliojitokeza kuchukua sare za shule zilizotolewa na shirika la MOCSO
………………………………….
Shirika lisilo la Serikali la MOCSO lililo na makazi yake Kiloleli kata ya Nyasaka wilaya ya Ilemela kupitia mradi wake wa Achieve limesaidia watoto wasiojiweza na kuishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa kuwapa Sare za shule, soksi, mabegi na mahitaji mengine ya shule ili kuweka mazingira rafiki na salama kwa wanafunzi wanaosoma shule za msingi na sekondari zinazopatikana ndani ya manispaa ya Ilemela na Jiji la Mwanza waweze kupata Elimu bila kikwazo cha aina yeyote
Akizungumza wakati wa zoezi la kukabidhi vifaa hivyo vya shule Afisa Msimamizi Mashauri ya watoto kutoka katika shirika la MOCSO Bwana Amos Jackson amesema kuwa shirika lake limekusudia kuwafikia watoto 315 wa shule za msingi na sekondari zilizopo katika manispaa ya Ilemela na Jiji la Mwanza kwaajili ya kuwapatia vifaa hivyo vya shule ili kuwapunguzia gharama wazazi na walezi wa watoto hao lakini pia kuweka mazingira rafiki yatakayosaidia watoto hao kupenda shule hivyo kupunguza utoro na kuongeza ufaulu
‘.. Lengo letu ni kuisaidia jamii hasa watoto waliopo katika mazingira hatarishi na makundi maalum katika kupunguza kero na changamoto zinazokwamisha kufikia ndoto zao ..’ Aisema
Aidha Bwana Amos amezitaka taasisi na mashirika mengine kuunga mkono jitihada za Serikali katika kupambana na changamoto zinazokabili jamii hasa watoto Kwa kuweka mazingira rafiki na salama lakini pia kuja na mikakati inayotekelezeka yenye lengo la kuisaidia jamii dhidi ya changamoto zinazoikabili
Kwa upande wake mratibu wa afya shuleni kutoka Manispaa ya Ilemela Bwana Finias Nyaganyi mbali na kulipongeza shirika la MOCSO kwa juhudi zake katika kuisaidia Serikali kupunguza kero na changamoto zinazokabili watoto amewaasa wanafunzi walionufaika na msaada huo kutunza na kutumia vizuri vifaa vya shule walivyokabidhiwa ili vikatekeleze lengo lililokusudiwa
Bi Stella Mbura ni Afisa Ustawi wa Jamii manispaa ya Ilemela ambapo amewahakikishia watoto kuwa Serikali inawajali na itaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kuwalinda na kuzuia vitendo vya ukatili kwa watoto sanjari na kuiasa jamii kuripoti na kuchukua hatua katika kudhibiti vitendo vya ukatili
Lucia Bugama ni manafunzi wa shule ya msingi Nyakato ‘A’ ambae amenufaika na msaada huo, Yeye amelishukuru shirika la MOCSO Kwa msaada walioutoa utakaosaidia kuwaondolea Adha ya ukosefu wa Sare za shule kwani wapo baadhi Yao waliokuwa wakishindwa kuhudhuria masomo kutokana na kukosa sare za shule na vifaa vyengine muhimu