Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Sophia Edward Mjema kufuatia vifo vya watu 16 vilivyotokea katika ajali ya gari.
Ajali hiyo imetokea tarehe 8 Agosti, 2022 katika kata ya Mwakata wilaya ya Kahama, Mkoani Shinyanga saa 4 usiku.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga ACP Leonard Nyandahu jumla ya waliopoteza maisha ni watu 16 (wanawake 2 na wanaume 14) na majeruhi 11 (wanawake 4 na wanaume 7) ambao wamepelekwa hospitali ya Kahama.
ACP Nyandahu amesema ajali hiyo imehusisha gari ndogo aina ya IST yenye namba ya usajili T 880 DUE iliyokuwa ikielekea Kahama na kuigonga kwa nyuma trekta iliyokuwa imebeba kuni yenye namba ya usajili T 719 AUP.
Watu watatu waliokuwa katika gari hiyo ya IST walifariki dunia papo hapo na dereva wa trekta kukimbia.
Aidha, basi dogo la abiria lenye namba za usajili T 350 DDX lililokuwa likitokea Kahama liligonga kwa mbele gari aina ya Scania yenye namba ya usajili T.658 DUW iliyokuwa imesimama eneo hilo la ajali na abiria 13 kufariki dunia papo hapo.
Aidha, Rais Samia amevitaka vyombo vyote vinavyosimamia usalama barabarani kuongeza juhudi za kudhibiti ajali.
Rais Samia pia anawapa pole wafiwa wote na anaungana na familia hizo katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
Mungu azilaze roho za marehemu wote mahali pema peponi. Amina.