Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilayani Igunga Mkoani Tabora Mhandisi Sebastian Marwa akisoma taarifa ya utekelezaji mradi wa Maji ya ziwa Viktoria katika Kijiji cha Bukoko kata ya Bukoko wilayani humo juzi kwa kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahili Nyanzabara.
************************
Na Lucas Raphael,Tabora
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Sahili Nyanzabara amepongeza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilayani Igunga Mkoani Tabora kwa kusimamia ipasavyo mradi wa maji ambao umewezesha wanakijiji zaidi ya 6,000 kupata maji safi ya bomba kwa mara ya kwanza.
Ametoa pongezi hizo jana wakati Mwenge wa Uhuru ulipofika katika Kijiji cha Mwazizi kata ya Bukoko wilayani humo na kushuhudia wakazi wa kijiji hicho wakifurahia maji hayo ambayo hawajawahi kuyaona tangu nchi ipate uhuru.
Alisema dhamira ya serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuona wakazi wa vijiji vyote wanapata huduma ya maji safi na salama ya bomba ili kumtua mama ndoo kichwani.
Aliongeza kuwa Mheshimiwa Rais amepeleka fedha nyingi katika halmashauri zote ili kufanikisha utekelezaji miradi hiyo lakini baadhi ya Watendaji wa RUWASA wamekuwa wakichelewesha miradi hiyo pasipo sababu yoyote.
‘Nawapongeza kwa kusimamia vizuri mradi huu, hakikisheni unawafikia wakazi wa vijiji vingine kama ilivyokusudiwa, ile dhana ya RUWASA maji bombani sasa naiona, mwenge wa uhuru umeridhia kuweka jiwe la msingi’, alisema.
Awali Meneja wa Wakala huo Wilayani hapa Mhandisi Sebastian Marwa alimweleza kuwa mradi huo ni mwendelezo wa utekelezaji mradi wa maji ya ziwa Viktoria ambao utafikisha huduma hiyo katika kata 2 za Bukoko na Mtunguru.
Alisema wakazi wa Vijiji 2 vya Mwazizi na Bukoko tayari wameanza kunufaika na huduma hiyo na awamu inayofuata ni kufikisha maji hayo katika Kijiji jirani cha Mtunguru kilichoko katika kata ya Mtunguru, kazi inaendelea kwa kasi.
Alibainisha lengo la mradi huo kuwa ni kufikisha huduma ya maji safi na salama ya bomba kwa wananchi wapatao 6,526 wanaoishi katika Vijiji vya Bukoko na Mtunguru na utagharimu kiasi cha sh mil 436.24.
Mbunge wa Jimbo la Igunga, Nicholous Ngasa alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapelekea kiasi cha sh mil 500 za UVIKO 19 katika Jimbo lake kwa ajili ya utekelezwaji mradi huo utakaonufaisha wakazi wa vijiji 3.