*************************
Ankara, Uturuki
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi Leo tarehe 7 Agosti, 2022 amekutana na kufanya mazungumzo na Watanzania wanaosoma na kufanya kazi nchini Uturuki wakiwemo madaktari.
Katika mkutano huo ambao uliwakutanisha pia Viongozi wa Dispora wa nchini humo uliofanyika Ofisi za Ubalozi wa Tanzania Ankra Uturuki ulikua na lengo la kupata uelewa kuhusu sekta ya Afya nchini humo na kuangalia nyanja ambazo Tanzania inaweza kufaidika nazo kutokana na mashirikiano baina ya nchi hizo mbili hususani kwenye sekta ya Afya.
Prof. Makubi alisema Serikali ya Tanzania imefanya jitihada kubwa katika kuboresha huduma za afya katika ngazi zote kuanzia ngazi ya afya ya msingi,ujenzi wa hospitali za Mikoa,Kanda (Mtwara na Chato), hospitali ya Kumbukumbu ya Mwl. Nyerere-Mara,ujenzi wa huduma za dharura(EMD) na wagonjwa mahututi(ICU),ujenzi wa majengo maalumu ya afya ya Uzazi, Mama na mtoto pamoja na ununuzi wa vifaa vya uchunguzi ikiwemo mashine za CT-Scan na MRI.
Aidha, Prof. Makubi alielezea maeneo ambayo Tanzania inapendekeza kushirikiana na Serikali ya Uturuki katika mafunzo ya wataalamu,kubadilishana uzoefu,uwekezaji katika huduma za tiba na ujenzi wa viwanda vya dawa pamoja na vifaa tiba.
Vile vile Katibu Mkuu huyo amewashukuru madaktari wa Kitanzania wanaofanya kazi nchini Uturuki kwa moyo wa kizalendo wa kujitoa kukutana naye na kujadiliana masuala mbalimbali ya kuboresha huduma za afya nchini Tanzania.
Kwa upande wao Diaspora hao wameshauri ili kuboresha huduma za afya nchini ni kupunguza gharama za mifuko ya Bima ya afya na kuongeza ufanisi ni vyema Wizara ya Afya ifikiria kuweka mfumo wa Ki-eletroniki utakaounganisha huduma zote za afya katika taasisi za umma na binafsi pamoja na mifuko ya Bima ili taarifa za mgonjwa ziweze kupatikana na kuwa na ulinganifu kutoka hospitali moja kwenda hospitali nyingine.
Hata hivyo wataalamu hao wameomba kuwepo na ulinganifu wa mitaala ya mafunzo ya afya ili kutambulika katika usajili wa viwango vyao vya utaalamu au ubingwa.
Masuala mengine yaliyojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na huduma za kibingwa zinazopatikana nchini Uturuki na hospitali zinazotoa huduma hizo na namna ambavyo Tanzania inaweza kuboresha huduma za afya kutokana na mashirikiano.
Akimkaribisha Katibu Mkuu huyo,Kaimu Balozi wa Tanzania nchini Uturuki Mhe. Iddi Mwamweta alitoa historia fupi ya ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Uturuki
Katika ziara hiyo Katibu Mkuu huyo aliambatana na Madaktari Bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, Taasisi ya Saratani Ocean Road, Taasisi ya Mifupa Muhimbili na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete.