Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula akihutubia waumini wa kanisa la Sabato hawapo pichani juu ya ushiriki wa Sensa ya Watu na Makazi
Mchungaji David Makoye akimuombea Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula na viongozi wengine wa nchi
***************************
Wananchi wametakiwa kushiriki na kutoa taarifa sahihi za Makazi na umiliki wake wakati wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika mapema mwezi Agosti 23 mwaka huu ili kupunguza migogoro ya ardhi inayoepukika
Rai hiyo imetolewa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa zoezi la ufungaji wa makambi katika kanisa la wasabato SDA lililopo Pasiansi wilaya ya Ilemela ambapo amewaasa kuhakikisha wanashiriki zoezi la Sensa ya Watu na Makazi sanjari na kutoa taarifa za umiliki wa Ardhi ili takwimu hizo ziweze kuisaidia Serikali kuzuia na kutatua migogoro inayohusu Ardhi ambayo imekuwa ikijitokeza bila sababu za msingi ikiwemo ile ya umiliki wa zaidi ya mtu mmoja
‘… Niwaombe mhakikishe mnatoa taarifa sahihi za sensa ya Makazi tukifanya hivyo tutaondoa migogoro isiyokuwa ya lazima katika sekta ya ardhi ..’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula amesisitiza waumini wa kanisa hilo kujibu maswali ya Sensa watakayoulizwa na makarani wa Sensa kwani kufanya hivyo ni takwa la kisheria sanjari na kuwaomba kuendelea kumuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hasan na Serikali anayoiongoza kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuwatumikia wananchi wake na kuwaletea maendeleo
Kwa upande wake Katibu wa Jimbo kuu la kaskazini mwa Tanzania kanisa la wasabato Mchungaji David Makoye Maduhu amesema kuwa kanisa linaridhishwa na Kasi ya utekelezaji washughuli za maendeleo pamoja na kushukuru kwa uwepo wa ulinzi na usalama kwani tangu kuanza kwa makambi hayo nchi nzima hakuna tukio lolote la uvunjifu wa amani lilijitokeza na kuripotiwa hivyo kushukuru Serikali na kuahidi kuendelea kuiombea
Mchungaji Nikodemas Ntabiudi ni Katibu wa Jimbo la Nyanza kusini wa kanisa la wasabato ambapo amempongeza Waziri Dkt Angeline Mabula kwa juhudi zake za kuwatumikia wananchi wa Jimbo lake licha ya kuwa na majukumu mengine ya kitaifa sanjari na ushirikiano anaoutoa kwa kanisa la wasabato kila wanapomuhitaji