***********************
Mkuu wa Wilaya ya Same, Mhe. Edward Mpogolo amewahamasisha vijana katika wilaya hiyo kushiriki zoezi la sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti 23 mwaka huu.
Wito huo umetolewa na Mhe. Mpogolo alipokua akizungumza na vijana zaidi ya 1800 waliokua kwenye kambi ya Kanisa la Waadventisti Wasabato Kanda ya Kaskazini iliyofanyika Alkanjenje wilayani hapo.
Vijana hao katika kambi hiyo walishiriki kwenye zoezi la uchangiaji damu kwa hiari na kupata chanjo ya uviko 19.
Mhe. Mpogolo akizungumza na vijana hao mbali na kuwapongeza kwa uchangiaji damu pamoja na kupata chanjo, amewataka kuendelea kutoa elimu kwa vijana wenzao walio mitaani umuhimu wa kupata chanjo.
Lengo la kuzungumza na vijana hao ni kuelimisha vijana kuanzia miaka 10-35 umuhimu wa sensa ya mwaka huu na kutoa elimu ya uviko 19 kwa vijana walioshiriki mafunzo hayo ambao wamechangia damu kwa hiari na kuchanja chanjo ya uviko 19 kwa wale wenye umri wa kuanzia miaka 18.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Miito na Malezi wa Kanisa la Advetist Wasabato Conference ya Kaskazini Mchungaji Mao alimshukuru Mkuu wa Wilaya kwa kuwatembelea Kambini na kutoa Elimu. Mchungaji Mao pia alimpongeza na kumuombea Dua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan. Alisema Rais Samia amekuwa kiungo kikubwa cha kujenga Umoja na Mshikamano Tanzania na wao kama Viongozi wa dini tutamuombea.