**********************
Na Joseph Lyimo
BAADHI ya wanawake wajawazito kwenye maeneo mbalimbali nchini wamekuwa wakilaumu kitendo cha baadhi ya wataaalam wa afya kuwalazimisha kupata kwanza chanjo ya UVIKO-19 ili waweze kupewa huduma mbalimbali za kiafya.
Wanawake hao wanaeleza kuwa wanatambua kuwa chanjo ya UVIKO-19 ni muhimu kwao katika kujilinda na janga la UVIKO-19 ila wanapata kikwazo kwa kulazimishwa na baadhi ya wataalam wa afya wachanje kwanza kabla ya kuhudumiwa.
Mkazi wa kata ya Kijungu Robert John anasema ni vyema wataalam wa afya wakatoa elimu kwa jamii ya eneo hilo hasa wanawake wajawazito katika kupata chanjo ya UVIKO-19 kuliko kuwalazimisha.
“Kwa kweli kila mmoja anatambua umuhimu wa kupata chanjo ya UVIKO-19 ili aweze kujikinga na janga hilo na pia chanjo hiyo inatolewa bila gharama, jamii ikipatiwa elimu inashiriki bila kulazimishwa kuchanjwa,” anasema John.
Mwanamke mjamzito mkazi wa kata ya Kijungu Mwanahamisi Juma anaeleza kuwa watumishi wa idara ya afya ambao siyo waaminifu wamekuwa wakiwaambia wajawazito wapate kwanza chanjo ya UVIKO-19 ndipo wapatiwe huduma nyingine.
Anaeleza kwamba mara baada ya Serikali kuwaagiza wataalam wa afya kuwa watu wa maeneo yao wanapaswa kupatiwa chanjo ya UVIKO-19 ndipo wao wakaamua kuwalazimisha wanawake wajawazito wapate chanjo.
“Hivi sasa sisi wanawake wajawazito tunatambua umuhimu wa chanjo mara baada ya kupatiwa elimu kuwa janga hilo ni hatari hivyo tuchanje, ni vyema wataalamu hao wakaendelea kutoa elimu kuliko kuwalazimisha watu wachanje,” anaeleza.
Mtaalamu wa ufuatiliaji na mdhibiti wa magonjwa wa Wizara ya Afya, Dkt Baraka Nzobo anasema kwamba maelekezo ya serikali ni kuwashawishi wananchi na kuwaelimisha wapate chanjo ya kujikinga na janga la UVIKO-19 na siyo kuwalamizisha wanawake wajawazito wachanjwe ndipo wahudumiwe.
“Mwanamke mjamzito anaruhusiwa kupata chanjo ya UVIKO-19 kwani hakuna madhara endapo akipata huduma hiyo ila kuchanja ni hiyari ya mtu na siyo kulazimishwa ili aweze kupata huduma hiyo,” anaeleza Dk Nzobo.
Anasema wanawake wajawazito kwenye maeneo mbalimbali nchini wamepewa elimu juu ya chanjo mbalimbali ikiwemo ya UVIKO-19 hivyo wanapaswa kuelimishwa na siyo kulazimishwa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI) Innocent Bashungwa amesema amepiga marufuku baadhi ya watoa huduma kuwalazimisha wanawake wajawazito kupata chanjo ya UVIKO-19 kabla ya kupatiwa huduma kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali.
Waziri Bashungwa anasema kuwa wanawake wajawazito hao wapewe elimu na ushawishi wa chanjo hiyo ili wafanye uamuzi wenyewe kwani chanjo ya UVIKO-19 ni hiyari siyo lazima.
Anasema baadhi ya wanawake wajamzito wamekuwa wanalalamika kulazimishwa kupata chanjo ya UVIKO-19 ili wapatiwe huduma mbalimbali ikiwemo kliniki, kwani wanapaswa kuamua wenyewe na siyo kulazimishwa.
“Kulikuwa na tabia ya kwenye baadhi ya maeneo nchini badala ya kutoa elimu na kuhamasisha wanawake wajawazito wapate chanjo ya UVIKO-19 wao wanawalazimisha kwa kuwapa masharti kuwa lazima wachanjwe kwanza ndipo wapatiwe tiba,” anasema Bashungwa.
Anaeleza kwamba kujikinga kwa kupata chanjo ya UVIKO-19 ni hiyari na siyo lazima hivyo watumishi wachache wasitoe maelekezo ya kwao na kubadili kuwa ni maelezo ya Serikali kuhusu chanjo hiyo.
“Hayo siyo maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan juu ya kuwapa chanjo ya UVIKO-19 wananchi wake, kwani wataalam wanapaswa kutoa elimu na kuwahamasisha na siyo kuwalazimisha wanawake wajawazito kupata chanjo hiyo,” anaeleza Waziri Bashungwa.
Waziri huyo amewaagiza viongozi wa Mkoa wa Manyara na Wilaya ya Kiteto kuhakikisha wanakwamisha matukio ya wanawake wajawazito kulazimishwa kupata chanjo ya UVIKO-19 ndipo wapate huduma kwenye eneo la kata ya Kijungu baada ya kusikia malalamiko hayo.
“Mkuu wa mkoa wa Manyara na mkuu wa wilaya ya Kiteto mhakikishe mnafuatilia hapa Kijungu endapokuna watumishi wachache wenye tabia hiyo waache mara moja,” anaeleza Waziri Bashungwa.
Anasema atawaachia wananchi wa eneo hilo la kata ya Kijungu namba yake ya simu ili waweze kumpigia simu endapo kutakuwa na watumishi wa idara ya afya wanaendelea na tabia hiyo ya kuwalazimisha.
Anasema wasiwepo wataalamu wachache wanaowashinikiza wanawake wajawazito kupata chanjo ya UVIKO-19 badala ya kuwapa elimu na ya faida ya na siyo kutaka kuwanyima huduma hadi wapate chanjo.
“Kila mtu anatambua kuwa chanjo ya UVIKO-19 ni hiyari na pale mtu anapochanja anakuwa ameongezea mwili wake nguvu za ziada ya kupambana dhidi ya janga la UVIKO-19 na siyo kulazimisha watu wachanje ndiyo wapatiwe huduma,” anaeleza Bashungwa.
Mkazi wa kata ya Kijungu Mariam Seleman amemshukuru Waziri Bashungwa kwa kutoa kauli hiyo kwani kuna baadhi ya wataalam wa idara ya afya walikuwa wanawalazimisha wanawake wapate chanjo hiyo ndipo watibiwe.
“Nadhani itakuwa mwisho kwa watumishi wa afya kutowalazimisha wanawake wajawazito wapate chanjo kwanza kabla ya kupata huduma kwani imetangazwa kuwa ni hiyari siyo lazima,” anaeleza Mariam.
Hata hivyo, mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Kiteto, Dkt Malkiadi Mbota anaeleza kuwa hakuwahi kupata malalamiko yoyote juu ya wanawake wajawazito kutakiwa kupata chanjo ya UVIKO-19 ili waweze kuhudumiwa.
Anaeleza kuwa Waziri alikuwa anatoa maelekezo ya jumla nchini kuwa tabia hiyo ameshalalamikiwa maeneo mengine ila ameyasemea Kiteto, ila baadhi ya watu wanazungumza tuu ili hali hawajawahi kuambiwa hivyo ila wanafuatilia hilo.
Kwa mujibu wa andiko la utafiti wa chuo kikuu cha Harvard cha Marekani, watu wenye mimba na ambao walikuwa na mimba hivi karibuni wana uwezekano mkubwa wa kuugua au kupelekwa hospitali dhidi ya UVIKO-19 ukilinganisha na watu wengine.
Utafiti huo unaeleza kuwa utoaji wa chanjo za UVIKO-19 unapaswa kutolewa ikiwemo dozi za nyongeza kwa watu ambao wana ujauzito, walikuwa wajawazito hivi karibuni ikiwemo wale ambao wananyonyesha, wanaojaribu kuwa wajawazito sasa, au watakuwa wajawazito hapo baadae.
Watu wenye matatizo ya kiafya ya muda mrefu, kama vile pumu, ugonjwa wa kisukari, au ugonjwa wa moyo au mapafu, wako katika hatari kubwa ya kuugua na UVIKO-19.