Faraja Lazaro Damasi
Josephat Joshua Gisemo
Yusufu Lucasi Changalawe
Kassim Selemani Mbundwike
……………………………….
Na Issa Michuzi, Birmingham
Leo Jumamosi Agosti 6, 2022 Tanzania inatupa karata zake nne za mwisho katika Michezo ya 22 ya Jumuiya ya Madola inayoendelea jijini Birmingham, Uingereza, wakati mabondia wake Wawili na wanariadha idadi hiyo hiyo wakiingia dimbani kupambania medali.
Kwa upande wa ndondi bondia Yusuf Lucasi Changalawe atapambana na Sean Lazzerini wa Scotland katika nusu finali ya kwanza ya uzani wa 75kg-80kg (Light Heavyweight ) katika Ukumbi Namba 4 wa National Exhibition Centre (NEC) majira ya saa 6:30 mchana kwa saa za Uingereza ama saa 8:30 mchana kwa saa za Tanzania.
Karata ya pili ya Tanzania itatupwa katika ndondi tena wakati bondia Kassim Selemani Mbundwike atakapopambana na Tiago Osorio Muxanga wq Msumbiji katika nusu finali ya pili ya uzani wa 67kg-71kg (Light Middle) katika Ukumbi huo huo wa NEC majira ya saa 10:45 za jioni saa za Uingereza ama saa 12:45 za jioni kwa saa za Tanzania.
Mshindi katika mapambano hayo mawili ya ndondi atatoa matumaini kwa Tanzania kupata medali ya Dhahabu ama ya Fedha, kulingana na matokeo ya mchezo wa fainali utakaocheza siku ya Jumapili, ambapo mshindi atabeba Dhahabu na wa pili ni Fedha.
Ikumbukwe kwamba hadi kufikia wakati huu wa Changalawe na Mbundwike kucheza hatua hiyo ya nusu finali leo kila mmoja wao tayari ana medali ya Shaba, kwani katika ndondi mabondia wote wanaofika hatua hiyo huwa moja kwa moja wanatunukiwa medali hiyo, hata kama watashindwa katika mchezao wao wa nusu fainali.
Karata zingine mbili zilizosalia wanazo wanariadha Josephat Joshua Gisemo na mwenzie Faraja Lazaro Damasi ambao watakuwa bega kwa bega katika dimba moja katika fainali ya mbio za mita 5,000 Uwanja wa Alexander mnamo majira ya saa 2:10 jioni kwa saa za Uingereza ama saa 4:10 Usiku kwa saa za Tanzania.
Gisemo na Damasi ni miongoni mwa wanariadha 20 kutoka nchi mbalimbali za Jumuiya ya Madola watakaowania medali za Dhahabu, Fedha na Shaba.
Kimsimamo, Tanzania inashika Nafasi ya 25 kati ya Nchi 35 ambazo zimeweza kuambulia medali hadi jana Ijumaa Agosti 5, 2022. Nafasi hiyo ya 25 inashikiliwa pia na Nchi zingine sita ambazo zimepata medali moja moja za Fedha kamą Tanzania. Nazo ni Barbados, Dominica, Guernsey, Papua New Guinea, St. Lucia na Gambia. Takriban wanamichezo 5,054 wanashiriki katika Michezo hiyo kutoka Nchi 72 ambapo jumla ya Michezo 20 huchezwa.
Jirani zetu Kenya ni wa 11 kimsimamo hadi jana kwa kuwa na jumla ya medali 9 ikiwa ni 2 za dhahabu, 3 za Fedha na 4 za Shaba. Uganda ni ya 21 kwa kuwa na Medali 2 za Dhahabu na moja ya Shaba.
Afrika Kusini na Nigeria ndio vingunge wa bara la Afrika katika kupata medali nyingi, ambapo hadi jana Ijumaa Afrika Kusini ilikuwa nafasi ya 7 kwa kusomba jumla ya medali 22 ambapo 7 ni za Dhahabu, 7 za Fedha na 8 za Shaba. Nigeria ni wa 9 kwa jumla ya medali 16, ambapo 7 ni Dhahabu, 3 ni Fedha na 6 ni Shaba.
Hadi jana Ijumaa nchi inayoongoza kwa wingi wa medali ni Australia yenye jumla ya medali 140, ambazo ni dhahahu 50, Fedha 44 na Shaba 46. Hao Wanafuatiwa na wenyeji Uingereza ambao hadi jana walikuwa na kumla ya medali 131 kiwa ni dhahabu 47, Fedha 46 na Shaba 38.
Hadi sasa Tanzania imeweza kujipatia jumla ya medali 22 (zote katika riadha na ndondi) katika Michezo hio ya Jumuiya ya Madola ambayo nchi imeshiriki michuano yote tokea inazishwe miaka 22 iliyopita, isipokuwa ya Mwaka 1968, na hadi sasa Tanzania inajivunia rekodi ambayo haijavunjwa hadi sasa ya mbio za mita 1,500 iliyowekwa Mwaka 1974 na Filbert Bayi jijini Christchurch, New Zealand.
Katika medali hizo 22, hadi jana Ijumaa Tanzania imeshinda 6 za Dhahabu, 7 za Fedha na 9 za Shaba.
Kuna kila dalili kwamba jedwali la Takwimu za medali za Tanzania huenda likabadilika kwa kushiba ifikapo mwisho wa wiki hii ambapo wachezaji wake hao wanne waliosalia watakuwa wameshahitimisha kazi waliyotumwa kuifanya Uingereza.