Na Mwandishi wetu, Chemba
MSANII maarufu Smaina na mwanamitindo maarufu Miriam Odemba, wanatarajiwa kunogesha Tamasha la Usandawe Festival, linalotarajiwa kufanyika kesho jumapili kwenye Kata ya Kwamtoro, Wilayani Chemba Mkoani Dodoma.
Mratibu wa tamasha hilo, msanii Smaina amesema mgeni rasmi wa tamasha hilo anatarajiwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Chemba, Mohammed Lujuo Monni.
Amesema kwenye tamasha hilo kutakuwa na burudani mbalimbali zitakazotolewa kwenye kijiji hicho cha Kwamtoro ikiwemo sanaa, michezo, elimu, afya na burudani.
“Tumeongozana na wasanii mbalimbali wa bongo Flava, waandishi wa habari na pia kutakuwa na kikundi cha ngoma za asili Landaa Culture Enseble kutoka Dar es salaam,” amesema Smaina.
Amesema wameshapata baraka za Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Simon Chacha ambaye aliwaunga mkono kwa kufurahia tamasha hilo kwani linatoa fursa mbalimbali kwa wananchi wa Chemba, baada ya kufika ofisini kwake.
“Niliongozana na Katibu wa Usandawe Festival Hamis Alagwa na tukafurahi kwa kitendo cha Mkuu wa Wilaya yetu ya Chemba kutuunga mkono kwenye tamasha hili,” amesema Smaina.
Mmoja kati ya wakazi wa Chemba Joseph Degera anaeleza kuwa anafurahia tamasha hilo kwani anatarajia kuona wasanii mbalimbali na kupata elimu na burudani kwenye tamasha la Usandawe Festival.
“Pia ninatarajia kumuona dada yetu Miriam Odemba ambaye baba yake ni mjaluo na mama yake ni msandawe, tukutane Usandawe Festival,” anasema Degera.