Na Prisca Libaga Maelezo Arusha
Jumuiya ya Afrika ya Mashariki(EAC) imepeleka waangalizi wa uchaguzi wapatao 52 katika uchaguzi Mkuu wa Kenya uliopangwa kufanyika Jumanne ijayo ya Agosti 09 ya Mwaka huu
Akipeperusha bendera ya jumuiya hiyo kuashiria kuanza kazi kwa waangalizi hao wa EAC jijini Nairobi leo kiongozi wa timu hiyo ya waangalizi hao Dkt Jakaya Kikwete amesema walipata mafunzo ya siku tano ya miongozo ya kimataifa ya uanguzi wa chaguzi kuu za nchi.
Dkt.Kikwete ambaye pia ni Rais Mstaafu wa Tanzania amebainisha kuwa jumla ya waangalizi 52 wa uchaguzi kutoka nchi wanachama wa EAC wanaogawanyika katika makundi 15 wakiwemo kutoka bunge la Afrika ya Mashariki(EALA) watakuwa waangalizi wa uchaguzi mkuu huo wa Kenya
Amesema kuwa majukumu ama kazi ya waangalizi hao ni pamoja na kufuatilia zoezi zima la kampeni,Kufuatilia zoezi la upigaji kura na usimamizi wa vituo vya kupigia kura na ujumlishaji wa matokeo na kutangazwa kwa matokeo
Waangalizi hao kutoka EAC wanatarajia kuandaa taarifa yao ya awali kwa kile katika mchakato wa uchaguzi huo walichoshuhudia ambayo itatolewa Agosti 11 ya Mwaka huu wa 2022