Mkuu wa Mkoa wa Singida, aliyemaliza muda wake Dk.Binilith Mahenge (kulia) akimkabidhi Mkuu Mpya wa Mkoa wa Singida, Peter Selukamba baadhiya nyakaraka wakati wa makabidhiano ya ofisi. |
Mkuu wa Mkoa wa Singida, aliyemaliza muda wake Dk.Binilith Mahenge (kulia) na Mkuu Mpya wa Mkoa wa Singida, Peter Selukamba wakisaini nyaraka mbalimbali wakati wa makabidhiano ya ofisi. |
Na Dotto Mwaibale, Singida
MKUU mpya wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba,amesema kuwa Mkurugenzi wa
Halmashauri atakayeshindwa kujibu hoja za ukaguzi hatakwenda likizo.
Serukamba alisema hayo jana wakati akizungumza na watendaji kutoka wilaya
zote za mkoa huu wakiwamo wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri baada
ya kukabidhiwa ofisi na aliyekuwa mkuu wa mkoa Singida Dk.Binilith Mahenge.
Kuhusu ukusanyaji wa mapato alisema kwamba atakachokiangalia ni mapato
halisi na sio asilimia zilizokusanywa.
“Tusipimane kwa ‘percentage’ tuangalie kiasi cha mapato
kilichokusanywa maana kuna mchezo wa halmashauri kuweka makadirio kidogo ya
ukusanyaji wa mapato na baadaye kuonekana makusanyo yaliyopatikana ni
mengi,” alisema.
Serukamba alisema atakaa na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi,Wenyeviti wa
halmashauri pamoja na madiwani kuangalia makadirio ya mapato yanayowekwa katika
kila halmashauri na namna ya kuyaongeza kila mwaka.
Kuhusu bima ya afya, alisema atahakikisha kila mwananchi anakuwa na kadi ya
bima ya afya ya CHF au NHIF ili waweze kupata huduma za matibabu bila usumbufu.
Serukamba alisisitiza suala la usafi wa mazingira kwa kila mji linapewa
kipaumbele pamoja watumishi wanakuwa wanadhifu wanapokwenda kazini.
“Usafi hauhitaji bajeti ya serikali ni utaratibu tu, haiwezekani
unakuja ofisini ukiwa umevaa malapa lazima tuhakikishe miji yetu inakuwa
misafi,” alisema.
Kuhusu kilimo alisema suala hili ataliwekea mkazo kwa kuhakikisha watu
wanalima kweli na kujiwekea malengo kila mwaka ili kuongeza uzalishaji wa
mazao.
Mambo mengine atakayoyashughulikia ni migogoro ya ardhi,anuani za makazi na
suala la amani usalama katika mkoa.
Naye Mkuu wa Mkoa aliyemaliza muda wake Dk. Mahenge, aliwashukru watumishi
wote wa Mkoa wa Singida kwa ushirikiano waliompa katika kipindi alichokuwa
mkoani hapa na kutaka ushirikiano huu wauonyeshe kwa RC Serukamba.
Dk.Mahenge alisema mtaji mkubwa wa maendeleo ni amani na usalama na kwamba
anashukru ameuacha mkoa ukiwa na amani.