Mkuu wa shule ya Hazina ya Magomeni jijini Dar es Salaam Omar Juma akimpa zawadi mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo, Iptusm Ramadhani kwa kuwa wa kwanza kwenye mtihani wa utamilifu shuleni hapo uliofanyika hivi karibuni na shule hiyo kufanikiwa kuwa ya kwanza wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam (PICHA: MPIGA PICHA WETU)
Mkuu wa shule ya msingi Hazina ya Magomeni Dar es Salaam, Omar Juma, akimpa zawadi mwanafunzi wa darasa la saba Cassie Mazwile, aliyeshika nafasi ya tatu shuleni hapo kwenye matokeo ya mtihani wa utamilifu (moko) uliofanyika hivi karibuni ambako shule hiyo ilishika nafasi ya kwanza wilaya ya Kinondoni MPIGA PICHA WETU
Mwalimu Mkuu wa shule ya Hazina, Omar Juma akiwa kwenye picha ya pamoja na wanafunzi wa shule hiyo baada ya shule yao kuwa ya kwanza kwenye mitihani ya utamilifu (moko) darasa la saba wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam
Wanafunzi wa shule ya msingi Hazina ya Magomeni jijini Dar es Salaam wakiwa kwenye picha ya pamoja na tuzo mbalimbali mara baada ya shule yao kuibuka ya kwanza wilaya ya Kinondoni kwenye matokeo ya mitihani ya utamilifu (moko), kwa darasa la saba iliyofanyika mwezi Julai mwaka huu
Na Mwandishi Wetu
SHULE ya Msingi Hazina ya Magomeni jijini Dar es Salaam, imeongoza kwenye matokeo ya mtihani wa utamilifu (Mock), darasa la saba kwa Wilaya ya Kinondoni.
Kwenye matokeo hayo yaliyotolewa na Mkoa wa Dar es Salaam, hivi karibuni, shule hiyo imeshika nafasi ya kwanza kati ya shule 158 za wilaya hiyo.
Mkuu wa shule hiyo, Omar Juma, alisema jana kuwa shule hiyo iliongoza kwenye mtihani uliofanyika mwezi wa nne na ule uliofanyika mwezi wa saba mwaka huu.
Alisema walimu wake wamekuwa wakijituma kuwaandaa wanafunzi hao kwaajili ya mitihani ya ndani na ile ya kitaifa na kwamba hiyo ndiyo imekuwa siri kubwa ya mafanikio kwao.
Alisema kutokana na maandalizi mazuri waliyoyafanya kwa wanafunzi hao wanaimani kwamba watafanya vizuri zaidi pia kwenye mtihani wa kitaifa wa darasa la saba mwaka huu.
“Sisi tunapiga kazi hapa ni kazi tu nawashukuru walimu kwa kuifanya shule hii kuongoza mtihani wa utamilifu kwa mara ya pili mfululizo hii inatupa moyo wa kuendelea kufanyakazi,” alisema Omar
Alisema kujituma kwa walimu na ushirikiano ambao wamekuwa wakiupata kwa uongozi wa shule na wanafunzi ndiyo kitu wanachojivunia.
“Walimu wanafanyakazi kwa moyo sana, wazazi wa wanafunzi wamekuwa wakitoa ushirikiano mzuri sana kwa shule na uongozi wa shule unawajali sana walimu, hayo kwa pamoja yamekuwa yakisaidia ufaulu wetu kuwa juu mwaka hadi mwaka,” alisema
Aliwapongeza wanafunzi kwa mafanikio hayo na kuwataka wasome kwa bidii ili hatimaye waweze kuendelea kuongoza kitaifa na Mkoa wa Dar es Salaam kwenye mitihani ijayo.