Mkurugenzi wa benki ya Letshego Bw.Omar Msangi na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Assemble insurance Bi.Tabu Masoud wakisaini mkataba wa makubaliano kushirikiana katika utoaji wa bima kwa jamii. Hafla hiyo imefanyika leo Agosti 5,2022 katika Ofisi za Letshego Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Assemble insurance Bi.Tabu Masoud akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano na benki ya Letshego leo Agosti 5,2022 katika ofisi za benki hiyo Jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi wa benki ya Letshego Bw.Omar Msangi akizungumza na waandishi wa habari katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano na kampuni ya Assemble Insurance leo Agosti 5,2022 katika ofisi za benki hiyo Jijini Dar es Salaam. Mkurugenzi wa benki ya Letshego Bw.Omar Msangi na Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Assemble insurance Bi.Tabu Masoud wakipeana pongezi mara baada ya kusaini mkataba wa makubaliano kushirikiana katika utoaji wa bima katika jamii. Hafla hiyo imefanyika leo Agosti 5,2022 katika ofisi za benki ya Letshego Jijini Dar es Salaam.
**************************
KAMPUNI ya Bima ya Assemble imeingia mkataba wa makubaliano na benki ya Letshego,katika kuhakikisha huduma za bima zinaendelea kukua na kuifikia jamii kwa kiwango kikubwa.
Akizungumza leo Agosti 5,2022 na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Assemble insurance Bi.Tabu Masoud amesema kupitia ushirikiano huo sasa bidhaa zote za bima za kampuni yake zitatolewa na benki hiyo ya Letshego kupitia matawi yake yaliyopo katika maeneo mbalimbali nchini.
“Tunaiunga mkono serikali kwa kupanua wigo wa huduma za bima ambapo pia lengo la serikali pamoja na kuongeza idadi ya wananchi wanaotumia bima, pia angalau sekta hiyo ichangie kwenye Pato la Taifa asilimia 10,”Amesema Bi.Tabu.
Amesema kupitia ushirikiano huo benki hiyo ya Letshego itauza bidhaa za bima kama vile bima ya afya, bima ya mali, bima ya moto ikiwemo bidhaa mpya inayotolewa na kampuni ya Assemble ya bima ya ustawi wa afya ya akili.
Aidha Bi.Tabu amesema kuwa kupitia benki hiyo huduma hizo za bima zitapatikana kupitia huduma ya mikopo nafuu na ya muda mfupi ambayo itamrahisisha mwananchi kupata huduma hiyo kwa urahisi zaidi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa benki ya Letshego Bw.Omar Msangi amesema benki hiyo itaweza kutoa huduma ya mkopo nafuu na ya muda mfupi hasa kipindi cha mwaka mmoja.
Amesema watashirikiana kwa kiasi kikubwa na kampuni ya Assemble Insurance katika kuhakikisha jamii inapata huduma inayoostahiri na nafuu isiyoweza kumkandamiza.
Amesema benki hiyo pia inatoa huduma ya mkopo fasta kwa wajasiriamali wadogo na wanatoa mikopo inayofikia hadi shilingi milioni 50.