Na Waandishi wetu, Dar
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula ameagana na mabalozi wa Sweden na Finland nchini, Mhe. Anders Sjöberg na Mhe. Riita Swan baada ya kumaliza muda wao wa utumishi nchini Tanzania.
Waziri Mulamula amewaaga mabalozi hao kwa nyakati tofauti leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ambapo amempongeza Balozi wa Sweden Mhe. Sjöberg kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kudumisha uhusiano kati ya nchi yake na Tanzania wakati wote wa uwakilishi hapa nchini.
Waziri Mulamula amempongeza Balozi wa Sweden kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kuendeleza uhusiano baina ya Sweden na Tanzania ambapo Sweden imekuwa na mchango mkubwa katika miradi ya maendeleo vijijini, biashara na uwekezaji pamoja na elimu.
“Biashara kati ya nchi zetu mbili bado ipo chini, hivyo nimemhimiza Mhe. Sjöberg pamoja na kuwa amemaliza muda wake wa uwakilishi aendelee kuwasihi wafanyabiashara kutoka Sweden kuja kuwekeza Tanzania,” amesema Balozi Mulamula
Waziri Mulamula amesema mbali na sekta za biashara na uwekezaji pamoja na elimu,Tanzania itaendelea kushirikiana na Sweden katika sekta za afya, nishati na utalii hasa katika kuitangaza filamu ya ‘The Royal Tour’.
Kuhusu ushirikiano wa Tanzania na Finland, Balozi Mulamula ameongeza kuwa Finland na Tanzania ni marafiki wa muda mrefu na wa karibu ambapo kupitia ushirikiano huo Finland imekuwa ikiiunga mkono Tanzania kwa misaada katika mradi wa ukusanyaji wa kodi pamoja na mradi wa kuendeleza misitu.
Kwa upande wake Balozi wa Sweden Mhe. Sjöberg ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano iliompatia wakati wote alipokuwa nchini akitekeleza majukumu yake ya kibalozi.
“Naondoka baada ya kumaliza muda wangu wa uwakilishi hapa Tanzania lakini kwa jinsi nilivyofanya kazi na watanzania, Tanzania ni sawa na nyumbani…….nafarijika pia kuona masuala ya utawala bora, amani na usalama pamoja na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi vikiwa vimeboreshwa kwa kiasi kikubwa,” amesema Balozi Sjöberg
Naye Balozi wa Finland, Mhe. Swan ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kumpa ushirikiano wa kutosha wakati wa kipindi chake cha uwakilishi hapa nchini.
Mhe. Swan ameelezea kufurahishwa na uhusiano mzuri uliopo baina ya Finland na Tanzania na amepongeza hatua mbalimbali ambazo Serikali ya Tanzania imeendelea kuzichukua katika kuimarisha diplomasia ya uchumi.
“Nimekuwa hapa nchi kwa zaidi ya miaka mitatu, mambo mengi yamebadilika kwa sasa nimefurahishwa na maboresho katika ukuaji na uboreshaji wa mazingira ya biashara na uwekezaji……naiona Tanzania ya mafanikio siku za karibuni,” amesema Balozi Swan.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza na Balozi wa Sweden nchini, Mhe. Anders Sjöberg katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akimuaga baada ya kumaliza muda wake wa utumishi nchini
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika picha ya pamoja na Balozi wa Sweden nchini, Mhe. Anders Sjöberg. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Swahiba Mndeme pamoja na Maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akimkabidhi zawadi ya picha na Balozi wa Finland nchini, Mhe. Riita Swan baada ya kumaliza muda wao wa uwakilishi nchini
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula katika mazungumzo na Balozi wa Finland nchini, Mhe. Riita Swan baada ya kumaliza muda wao wa uwakilishi nchini
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akiagana na Balozi wa Finland nchini, Mhe. Riita Swan baada ya kumaliza muda wao wa uwakilishi nchini