MJUMBE wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga kupitia Kata ya Kilago,Khamis Mgeja amesema uchaguzi wa ndani wa CCM unaofanyika sasa unalenga kupanga usajili mpya wa viongozi kwa uchaguzi mkuu wa 2025.
Amesema uchaguzi huo wa viongozi wa CCM kuanzia ngazi za mashina hadi taifa,sasa umefikia ngazi ya kata na lengo lake kubwa ni kuhakikisha kinapata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu ujao baada ya kuchagua viongozi wenye sifa,waadilifu na wenye uwezo wa kuwatumikia wananchi.
Mgeja aliyasema hayo katika Mkutano Mkuu wa CCM Kata ya Kilago uliofanyika jana sambamba na uchaguzi wa viongozi wa kata hiyo ambapo alipita bila ya kupingwa katika nafasi ya ujumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM mkoa kupitia kata hiyo.
Katika uchaguzi huo Mgeja alipigiwa kura 120 na wajumbe wa mkutano huo na hivyo kutangazwa mshindi wa nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho ngazi ya Mkoa kutoka Kata ya Kilago, anapotoka.
Aidha msimamizi uchaguzi huo Hamisa Kalinga ambaye ni Diwani wa Viti Maalumu Kata ya Bulyanhulu, Halmashauri ya Msalala,alisema kuwa uchaguzi huo umefanyika vizuri na kuwasifu wanachama kwa utulivu tagu mwanzo wa hadi mwisho wa uchaguzi.
Mwansiasa huyo mkongwe baada ya matokeo amesema chaguzi za ndani ya CCM zinaendelea vizuri na demokrasia imetamalaki vizuri chini ya uongozi bora na imara uliotukuka wa Mwenyekiti wa CCM, Mama yetu Samia Suluhu Hassan na kuhakikisha kila mwanachama anapata haki ya kugombea.
“Nawaomba sana wanachama wote wa CCM nchini tumpongeze na tumuunge mkono mwenyekiti wetu wa taifa na wasaidizi wake kwa namna wanavyokiendesha Chama, sote ni mashahidi hakuna mwanachama anakosa haki ya kugombea na kuchagua kiongozi anayemtaka,”alisema Mgeja.
Pia kuelekea uchaguzi mkuu ujao Mgeja amewasihi na kuwataka wale wote ambao hawakubahatika kupata nafasi kutokata tamaa kwani CCM bado ina fursa nyingi kwa wanachama wake kupata uongozi katika nyadhifa mbalimbali siku zijazo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Kata ya Kilago, Hungwi Mabula amekisifu chama hicho kwa kutoa fursa na haki kwa kila mwanachama wake kugombea nyadhifa mbalimbali na hivyo kuleta usawa na kuondoa manung’uniko kwa wanachama wake.
Wakati huo huo Mkutano Mkuu wa Kata ya Kilago umempongeza Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha na kutekeleza miradi mingi ya maendeleo nchini pamoja na kuwa namba moja katika kuhangaika kutafuta fedha za miradi ya maendeleo kwa ajili ya wananchi .
Wajumbe hao wamesema Mwenyekiti huyo wa CCM Taifa ameleta miradi mingi nchini ikiwemo ya ujenzi wa madarasa 15,000 na kuhakikisha mwanafunzi kuanzia darasa la awali hadi kidato cha sita anasoma bure hali itakayowapa mwamko wananchi wengi hasa wa pembezoni kuwapeleka watoto wao shule.