Mkurugenzi wa Oryx Kalpesh Mehta (wa pili kushoto) akieleza jambo katika Kongamano la Nishati Tanzania ambalo linafanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.Mkurugenzi Mtendaji Oryx nchini Kalpesh Mehta, (wa pili kulia), akizungumza jambo na Mkurugenzi Mtendaji wa Beki ya CRDB, Abdulmajidi Nsekela,( kulia) alipotembelea kwenye banda hilo katika kongamano la nishati Tanzania linalofanyika jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja wa B2B Harriet Wandira.
Mkurugenzi Mtendaji Oryx, Kalpesh Mehta, (katikati), akizungumza na wadau wa nishati waliotembelea Banda la oryx kwenye kongamano la nishati nchini linalofanyika jijini Dar es Salaam
*****************
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI inayojihusisha na Biashara ya uuzaji wa nishati ya gesi na mafuta nchini Tanzania ya Oryx imesema ushirikiano, ubunifu pamoja na mbinu za kisasa kwenye usimamizi wa sekta ya nishati nchini utafanikisha sekta hiyo kuwa inendelevu na salama.
Hayo yameeelezwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Oryx nchini Kalpesh Mehta alipokuwa akichangia mjadala kwenye Kongamano la Nishati Tanzania linalofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIC), jijini Dar es Salaam.
“Sekta ya nishati ni kubwa na muhimu kwa maendeleo, jamii na uchumi wa nchi na watu wake hivyo njia ya kufanikisha sekta hiyo ni kuwekeza katika kila eneo,”amesema.
Mehta amesema matamanio ya Tanzania ni makubwa kupitia sekta hiyo na njia mojawapo ya kukidhi matamanio hayo ni kuwepo na mazingira rafiki na endelevu.
Akifafanua zaidi wakati wa majadiliano hayo amesema sekta hiyo ni muhimu katika maendeleo ya nchi na kwamba uendelevu wake unakuwepo kwa wahusika na sekta hiyo kutumia vipawa vyao, mbinu za kisasa na ushirikiano.
Mehta amesema hitaji la dunia ni kuona matumizi ya nishati safi, salama na endelevu yanaongezeka, hivyo kinachohitajika ni waliopo katika sekta hiyo kuwa sehemu ya mabadiliko.
“Ajenda kuu ya dunia ni kuona namna gani nishati jadidifu inapewa kipaumbele.Ni vema watu wote wenye vipawa na wabunifu kuonesha uwezo wao kuhakikisha sekta hiyo inapiga hatua chanya,” alisema.
Mkurugenzi huyo amesema iwapo wadau wote kuanzia Serikali, sekta binafsi na watumiaji wa rasilimali zinatokana na nishati watakuwa kitu kimoja ni wazi sekta hiyo itakuwa endelevu.
Amesisitiza ni vema msukumo ukaongezeka katika uwekezaji kwenye maeneo ambayo yataweza kuzalisha nishati ambayo ni safi na salama huku akieleza changamoto ya watu wenye kukidhi soko la ajira kwenye eneo hilo ni kubwa, hivyo juhudi zinahitajika ili kuziba pengo hilo.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), Suzan Ndomba amesema taasisi yao imekuwa ikishirikiana na waajiri kuhakikisha mazingira rafiki ya kutekeleza miradi yenye mwelekeo wa nishati safi na salama.
Ameongeza juhudi zao zimejikita katika kuhakikisha elimu inatolewa, ikiwemo na kuweka msukumo wa kupata mitaala yenye kukidhi soko la ajira.