Na. WAF – Manyara
Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe ameupongeza Uongozi wa Hospitali ya Misheni ya Haydom iliyoko Mkoani Manyara kwa kazi nzuri wanayofanya katika kuwahudumia wanachi na kuwataka kuendelea kutoa huduma bora za afya.
Dkt. Sichalwe ameyasema hayo Mkoani Manyara alipotembelea Hospitali hiyo kujionea hali ya utoaji wa huduma za afya ambapo amewataka kuwa na dawati la huduma kwa mteja ili kuleta ufanisi mzuri katika kutoa huduma.
Aliendelea kusisitiza kuwa, sababu za hospitali nyingi kushindwa kufanya vizuri ni pamoja na kukosekana uongozi mzuri katika utendaji, kutobadili fikra na tabia zinazodumaza maendeleo katika utoaji huduma kwa wananchi.
“Nahitaji wataalamu wa afya mrudi katika miiko yenu na weledi wenu hii itaturudishia hadhi ya taaluma na kuleta ufanisi mzuri wakati wa kutoa huduma kwa wananchi.”Amesema.
Hata hivyo Dkt. Sichalwe amewakumbusha watumishi katika hospitali hiyo kutumia fursa iliyotolewa na Serikali ya kujiendeleza kielimu ili kuendelea kupata ujuzi zaidi katika taaluma zao.
Aidha amewataka kuwasimamia vizuri na kwa karibu madaktari watarajali wanaofanya mazoezi kwa vitendo (Interns), kwa kuwaelekeza miiko ya taaluma na kufanya kazi kwa juhudi na ufanisi ili wapate ujuzi mzuri wa kulitumikia Taifa utaoleta matokeo chanya.