Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Wizara ya Maji, Simon Nkanyemka akizungumza wakati akihitisha mafunzo ya Quality Management System (QMS) kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji yaliyofanyika jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi Rasilimali za Maji Wizara ya Maji, Robert Sunday akizingumza katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya Quality Management System (QMS) yaliyofanyika jijini Dodoma.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo ya mafunzo ya awamu ya nne ya Quality Management System (QMS) yaliyofanyika jijini Dodoma.
Mwakilishi wa mabonde, Paschal Kutaw kutoka Bodi ya Maji ya Bonde la Wami-Ruvu
akitoa taarifa ya mafunzo ya Quality Management System (QMS) yaliyofanyika jijini
Dodoma.
Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Ujerumani (GiZ), Sylvand Kamugisha akizungumza katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya Quality Management System (QMS) yaliyofanyika jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Wizara ya Maji, Simon Nkanyemka akitoa cheti kwa Perpetua Massaga kutoka Bodi ya Maji ya Bonde la Ziwa Victoria miongoni mwa washiriki wa mafunzo ya Quality Management System (QMS) yaliyofanyika jijini Dodoma.
Mgeni rasmi, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Wizara ya Maji, Simon Nkanyemka akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa mafunzo ya Quality Management System (QMS) yaliyofanyika jijini Dodoma.
…………………………………………….
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Wizara ya Maji, Simon Nkanyemka amesema Serikali imeanza rasmi matumizi ya mfumo wa uthibiti ubora wa takwimu za rasilimali za maji –Quality Management System (QMS) kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wa bodi za maji za mabonde nchini.
Nkanyemka amesema mfumo huo umeanza kutumika rasmi Julai Mosi, 2022 na kila Bodi ya Maji ya Bonde inaendelea kutoa taarifa ya utekelezaji wake wa kila wiki. Nkanyemka ameyasema hayo wakati akihitimisha mafunzo Quality Management (QMS) yalioandaliwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) pamoja na Shirika la Kimataifa la Ujerumani (GiZ) yaliyofanyika jijini Dodoma.
Akihitimisha mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, amesema kuwa lengo kuu la mafunzo ya QMS ni kuboresha utendaji wa shughuli ya msingi za mabonde ya usimamizi na uendelezaji wa rasilimali za maji kwa kutumia takwimu sahihi za wingi na ubora zitakazofanikisha kutimiza malengo ya Serikali ya muda mfupi, kati na mrefu.
“Jukumu la msingi la Wizara ya Maji ni kusimamia Sera na Sheria katika kuhakikisha upatikanaji wa huduma ya maji ya uhakika mijini na vijijini, jukumu ambalo litafanikiwa kuweka mikakati madhubuti ya usimamizi wa rasilimali za maji kwa kuwa na takwimu sahihi zitakazosaidia kutimiza malengo ya Wizara”, Nkanyemka amefafanua.
“Kwa kulitambua hilo Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Ujerumani (GiZ) limeandaa mafunzo hayo ili kuimarisha eneo la ukusanyaji wa takwimu sahihi za hali ya maji, hatua itakayowawezesha mabonde yote yaweze kupata vyeti vya ithibati vya ubora utakaotokana ufanisi wa mabonde hayo”, Nkanyemka amesema.
Mkurugenzi Nkanyemka amesema mfumo huo utakuwa mwarobaini wa baadhi ya changamoto ikiwemo ukusanyaji hafifu wa maduhuli kupitia ukusanyaji wa takwimu sahihi za watumia maji, ambazo zitainua kiwango cha ukusanyaji wa maduhuli yatakayotumika kuimarisha shughuli za usimamizi wa rasilimali za maji kwenye ngazi za mabonde.
Awali, Kaimu Mkurugenzi Rasilimali za Maji Wizara ya Maji, Robert Sunday amesema mafunzo hayo yamekuwa na mafanikio makubwa ambapo washiriki zaidi ya 200 wameshiriki na kufuzu mafunzo hayo, nyaraka 373 za QMS zimeandaliwa na zimeanza kutumika rasmi pamoja na utekelezaji rasmi wa QMS kwa mabonde yote tisa nchini ambayo ni Bodi za Maji za Mabonde ya Rufiji, Wami-Ruvu, Kati, Ruvuma na Pwani ya Kusini, Mto Pangani, Ziwa Victoria, Ziwa Tanganyika, Ziwa Rukwa na Ziwa Nyasa.
Akizungumza kwa niaba ya wawakilishi wa mabonde, Paschal Kutaw kutoka Bodi ya Maji ya Bonde la Wami-Ruvu amesema washiriki wamepata mafunzo ya kufanya ukaguzi wa ndani wa QMS kwa kufuata mwongozo wa Shirika ka Viwango Duniani (ISO) 9001:2015, akisisitiza kuwa mafunzo hayo yataboresha utendaji wa kazi katika ukusanyaji, uchakataji na uandaaaji wa taarifa za rasilimali za maji katika mabonde.
Quality Management Assesment (QMS) ni mfumo wa kuboresha utendaji kazi wa ukusanyaji, uchakataji wa takwimu na utoaji wa taarifa ya rasimali maji katika mabonde ili kukidhi viwango kutokana na miongozo mbalimbali iliyopo ndani na nje ya nchi.
Mafunzo ya QMS yamefanyika kwa awamu nne katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Morogoro na Kilimanjaro kuanzia mwezi Aprili – Julai, 2022 yaliyoshirikisha zaidi ya washiriki 200 kutoka makao makuu Wizara ya Maji na mabonde tisa ya maji nchini.