Na Joseph Lyimo
MKOA wa Manyara, unazidi kupiga hatua kwenye suala zima la chanjo ya UVIKO-19 baada ya watu 200,000 kati ya walengwa 669,516 kupatiwa chanjo ya kujikinga na maambukizi ya jangwa la UVIKO-19.
Mganga mkuu wa Mkoa wa Manyara, (RMO) Dkt Damas Kayera anasema kwamba wamepanga mikakati ya kutumia njia nne ili kupata matokeo makubwa zaidi kwa watu kupata chanjo ya UVIKO-19.
Dkt Kayera anaeleza kuwa mwitikio wa wananchi wa mkoa huo kushiriki chanjo ya UVIKO-19 ni mkubwa ndiyo sababu wamefikia hatua hiyo ya watu 200,000 kushiriki kupatiwa chanjo hiyo.
Anasema kwamba hadi hivi sasa wamefikia asilimia 32 ya wananchi wa mkoa wa Manyara kupata chanjo ya UVIKO-19 kati ya walengwa 669,516 wanaotarajiwa kupatiwa chanjo mwaka huu.
Anasema kuwa hadi kufikia mwisho wa mwezi Julai mwaka huu wa 2022 wanatarajia kufikia asilimia 40 ya watu waliopatiwa chanjo ya UVIKO-19 kwa wananchi wa mkoa wa Manyara.
“Tunatarajia kutoa chanjo na kupata matokeo makubwa kupitia nyumba kwa nyumba na kufikia asilimia 40 ya lengo mwishoni mwa mwezi huu wa saba mwezi Julai,” anasema Dkt Kayera.
Anasema elimu imezidi kutolewa kwa wananchi mbalimbali wa mkoa huo ikiwemo kwenye shule za msingi, sekondari, vyuo, nyumba za ibada, masoko na magulio na maeneo mbalimbali ya mkoa wa Manyara.
Anasema kwamba mwitikio ni mkubwa kwani viongozi wa serikali na kijamii wamehamasika na waliochanjwa wapo salama hivyo wananchi wameona mfano kwa wahusika hivyo na wao wanashiriki kupata chanjo hiyo.
“Hivi sasa tumepanga kutoa chanjo kwa matokeo makubwa tukitumia njia nne, ili kuweza kufikia malengo tuliyojiwekea kwa walengwa hao 669,516 kupatiwa chanjo ya UVIKO-19 kwenye mkoa wetu,” anaeleza Dk Kayera.
Anataja miongoni mwa njia hizo nne walizojipanga nazo ni watoa huduma kuanzia kazi hiyo kutoka kwenye vituo vyao vya kutoa huduma na kuelekea nyumba kwa nyumba ili kufanikisha shughuli hiyo.
“kwenye mikusanyiko katika nyumba za ibada ikiwemo makanisani na misikitini na kwenye masoko na magulio tutawafuata watu huko kupitia watoa huduma na watawachanja huko huko,” anasema Dkt Kayera.
Anaeleza kwamba endapo sehemu za kutoa huduma ni mbali wataenda na kuwafuata wananchi huko kuliko kuwasubiria watoke majumbani mwao endapo itatokea kuwa na kikwazo hicho.
“Hivi sasa tumeungana kwa viongozi wa kijamii na serikali wote kwa pamoja tumeungana katika kushiriki kuhamasisha wananchi kuliko kutegemea wataalam wa afya wafanye hivyo peke yao,” anaeleza Dkt Kayera.
Mkuu wa mkoa wa Manyara (RC), Charles Makongoro Nyerere ametaka elimu kutolewa kwa wananchi ili kuondoa dhana potofu zilizojengeka miongoni mwao na kusababisha baadhi ya wananchi wasishiriki kupata chanjo ya UVIKO-19.
“Natoa wito kwa viongozi wote wakiwemo wakuu wa wilaya, wakurugenzi, wenyeviti wa halmashauri, madiwani, wenyeviti wa vijiji na vitongoji, viongozi wa dini, wazee wa kimila na jamii kwa ujummla kushirikiana kuhakikisha wananchi wanapata chanjo ya UVIKO-19 ,” anasema RC Makongoro.
Makongoro anasema kwamba viongozi wa dini wakitumia nyumba za ibada na kutoa elimu kwa waumini wao waondokane na mawazo potofu waende kuchanja ili kupata kinga ya UVIKO-19 kwani lengo la Serikali ni kuhakikisha inalinda afya zao.
Anasema viongozi wa kimila wana ushawishi mkubwa pia kwa jamii katika kuhakikisha wanawaelimisha wananchi wa maeneo yao kuwa Serikali haina nia mbaya katika kutoa chanjo ya UVIKO-19 hivyo jamii iepuke dhana potofu.
Mkazi wa kata ya Sanu Wilayani Mbulu Martin Nakei, mwenye umri wa miaka 46 anasema kuwa amepata chanjo ya UVIKO-19 mara baada ya kuona baadhi ya marafiki zake waliokuwa wabishi kupatiwa chanjo walivyopoteza maisha.
“Suala la changamoto ya kupumua lisikilize kwa jirani pekee kwani likikutokea utapata tabu kweli kweli kuna jamaa zangu walikuwa wabishi kupatiwa chanjo ya UVIKO-19 ila walipokamatwa nayo walipata shida mno,” anasema Nakei.
Anasema wengine walifariki dunia na wengine walipona na kuwaeleza watu kuwa suala la kushiriki chanjo ya UVIKO-19 lisiwe na ubishi kwani wataalam wa afya wameshatoa elimu ya kutosha.
Mkazi wa Mrara mjini Babati, Joyce Sanka mwenye umri wa miaka 55 anasema yeye binafsi ameshiriki kupata chanjo ya UVIKO-19 baada ya wataalam wa afya kumpa elimu na kubaini kwamba Serikali haiwezi kutoa kinga kwa watu kisha wapate madhara.
Sanka anaeleza kuwa yeye na familia yake akiwemo mume wake na watoto wake wawili walio na zaidi ya miaka 18 walipata chanjo hiyo na wanamshukuru Mungu hawakupata maambukizo ya UVIKO-19.
“Tulipewa elimu kuwa tunapatiwa chanjo ya UVIKO-19 ila siyo kinga kamili ya kupata maambukizi ya virusi hivyo na endapo tutaambukizwa hatutapata athari kubwa ila tunashukuru hatukupata changamoto hiyo,” anaeleza Sanka.
Mlipuko wa kwanza wa UVIKO-19 umetajwa kuanzia kwenye soko la Wuhan nchini China mwaka 2019 na hapa nchini uliingia mwaka 2020, ambapo mgonjwa wa kwanza alipatikana akiwa ni mwenyeji wa jijini Arusha.
Kwa mujibu wa andiko la chuo kikuu cha Johns Hopkins cha Marekani, watu milioni 550 wamethibitika kupata maambukizi ya UVIKO-19 duniani kote.
Kwa mujibu wa chuo hicho, hadi kufikia mwezi Julai mwaka 2022 zaidi ya watu milioni 6.3 wamefariki kutokana na maambukizi ya UVIKO-19 duniani kote.
Dalili za kawaida za UVIKO-19 ni homa, uchovu na kikohozi kikavu, baadhi ya wagonjwa wanaweza kuwa na maumivu na uchungu, kubanwa pua, kutokwa kamasi, vidonda kooni au kuhara.
Mara nyingi dalili hizi huwa si kali na huanza polepole, watu wengine huambukizwa lakini hawaonyeshi dalili zozote na huwa hawajisikii vibaya.
Watu wengi (takribani asilimia 80) hupona kutokana na ugonjwa huu bila kuhitaji matibabu maalum, ni kama mtu mmoja kati ya watu sita wanaopata UVIKO-19 ndiye hudhoofika na kutatizika kupumua.