Mstahiki Meya wa halmashauri ya manispaa Tabora Ramadhan Shabani Kapela akiongea katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya manispaa hiyo
………………………………………………..
Na Lucas Raphael,Tabora.
JESHI la Polisi Mkoani hapa limepongezwa kwa kuchukua hatua za haraka kudhibiti vibaka waliokuwa wakijihusisha na vitendo vya utekaji, uporaji na wizi wa bodaboda.
Vitendo hivyo ambavyo vilikuwa vimekithiri katika kata za Ndevelwa na Ifucha katika manispaa hiyo vilipelekea watu wengi kuporwa mali zao ikiwemo utekaji na kunyang’anywa bodaboda .
Pongezi hizo zimetolewa jana na Mstahiki Meya wa halmashauri ya manispaa Tabora Ramadhan Kapela katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo baada ya Jeshi hilo kuwasilisha taarifa ikibainisha hatua zilizochukuliwa kuthibiti vitendo hivyo.
Alisema matukio ya utekaji na uporaji mali za wananchi katika kata hizo yalileta hofu kubwa miongoni mwa jamii hali iliyopelekea kuwepo kwa malalamiko mengi ya wananchi.
‘Tunawapongeza sana askari wetu kwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo katika hili la kudhibiti vitendo viovu vinavyofanywa na baadhi ya watu wasiowatakia mema wenzao’, alisema.
Meya aliwataka Watendaji wa Vijiji na Kata ambao ndio Wenyeviti wa Kamati za Ulinzi za vijiji na Kata kuimarisha ulinzi shirikishi katika maeneo yao.
Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi hilo Wilayani Tabora George Bagyemu alisema walifanya msako mkali katika kata hizo na kufanikiwa kukamata watuhumiwa zaidi ya 5 waliokuwa wakijihusisha na vitendo hivyo.
Alisema maeneo yote yaliyokuwa yakilalamikiwa kwa kukithiri vitendo hivyo hususani eneo la Kazima hali sasa ni shwari na watuhumiwa waliokamatwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani muda wowote.
Awali akitoa malalamiko ya vitendo hivyo katika kikao hicho diwani wa kata ya Ifucha, Rose Kilimba alisema vitendo hivyo hadi sasa vimepoteza maisha ya mtu 1 na kujeruhi zaidi ya watu 5 ikiwemo kuporwa pikipiki.
Aliomba hatua zaidi kuendelea kuchukuliwa ili kukomesha vitendo hivyo ambavyo vinarudisha nyuma maendeleo ya wananchi.